2015-03-23 09:19:00

Watoto wanabebeshwa silaha kupigana Sudan ya Kusini


Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF linabainisha kwamba, licha ya juhudi za Jumuiya ya Kimataifa kuwaokoa watoto wanaoandikishwa kwenye majeshi ya waasi, lakini bado kuna idadi kubwa ya watoto ambao wanapelekwa mstari wa mbele kupigana Sudan ya Kusini.

 

Taarifa za UNICEF zinaonesha kwamba,  tangu mwaka 2013 hadi wakati huu kuna jumla ya watoto 12, 000 ambao wamekuwa wakitumiwa na majeshi ya Serikali na Waasi katika mapigano, jambo ambalo ni kinyume kabisa cha haki msingi ya watoto na sheria za kimataifa. Kutokana na hali tete ya kinzani nchini Sudan kwa kugombania madaraka, inahofiwa kwamba, watoto wengi wanaweza kuandikishwa kwenye majeshi ili kupelekwa mstari wa mbele.

 

Wasi wasi huu pia umeoneshwa na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutaka viongozi wakuu wa Sudan ya Kusini wanaoendelea kuchochea vita wawekewe vikwazo na Jumuiya ya Kimataifa. Watoto wanaotumiwa vitani kwa sasa ni changamoto kubwa kwa Umoja wa Mataifa, kama anavyosema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.