2015-03-23 16:36:00

Tafakari ya Jumapili ya tano ya Kipindi cha Kwaresima


Mpendwa mwana wa Mungu hatuachi kuendela katika safari ya wokovu tukifiri na kuwaza na kisha kupembua nini Mungu anataka tufanye kwa njia ya Neno lake. Katika Dominika hii ya tano ujumbe wa Neno la Mungu umezama katika ukuu wa upendo. Wale wote wampendao Mungu na viumbe vyake na zaidi mwanadamu wanahesabiwa haki katika yeye.

Kwa njia ya Nabii Yeremia Mungu anatangaza agano jipya ambalo litakuwa kwa ajili ya wote. Tunatambua kuwa alikwisha fanya agano na wana wa Israeli lakini kwa sababu ya dhambi zao walilivunja. Halikuwa limeandikwa mioyoni mwao bali kwenye mawe. Kumbe sasa atatia sheria yake mioyoni mwao na hivi hakutakuwa na haja ya mtu kufundishwa na mtu mwingine bali Mungu mwenyewe moja kwa moja atamfunza mtu kadiri apendavyo. Kwa njia ya agano hili Mungu atasamehe uovu wote.

Uaguzi huu wa Nabii Yeremia umekamilika katika ujio wa Masiha Yesu Kristu Mkombozi. Masiha hufanya kazi kwa njia ya Roho Mtakatifu na hivi sauti ya agano lake iko katika moyo wa kila mtu. Mtu atavutwa na sheria toka ndani na si nje na hivi uwezo wa kupambana na mwovu upo moyoni mwa mtu daima. Uwepo wake si jambo tu la kusema basi atafanya kazi mwenyewe bali kila mtu anapaswa kumpa ushirikiano katika uhuru wa wana wa Mungu ili ndipo matunda yazaliwe.

Somo la pili kutoka katika barua kwa Waebrania na latufundisha unyenyekevu na utii wa Yesu Kristu kwa Baba yake. Suala hili laonesha Umungu mtu wake. Kwa sababu ya utii na uchamungu wake sala yake daima inasikilizwa. Utii wa Bwana kwa Baba yake ni kwa njia ya mateso ambayo yamemkamilisha na hivi katika ukamilifu huo anakuwa chanzo kwa wokovu wa milele kwa watu wote.

Mwinjili Yohane anatangaza utilimilifu wa saa ya kutukuzwa Mwana wa Adamu kwa njia ya mateso na kifo cha Msalaba. Kifo cha Yesu ni mbegu ya uzima wa milele, matunda matakatifu ya ujio wa Mwana wa Mungu hapa duniani. Kama vile ambavyo Bwana amekubali kudharauliwa hapa duniani, Mungu amemwadhimisha mno na kumpa ukuu wa mbinguni.  Basi mpendwa, mwinjili ataka kutufundisha kuwa kwa kukubali dharau yaani kuichukia nafsi yetu kwa ajili ya wokovu, kwa ajili ya mashauri ya Injili tutaweza kupata uzima wa milele. Kuchukia nafsi ni kuweka nguvu yako katika utume wa kimisionari badala ya kujihurumia, ni kutaka kutumikia ufalme wa Mungu daima.

Mfano dhahiri na mkamilifu ni pale tunapomwona Bwana anavyojiweka mikononi mwa Baba yake akisema “Baba uniokoe katika saa hii lakini iwe ni kwa sifa na utukufu wako Baba! Daima kumbe sala yetu lazima ianze na sifa kwa Baba na mambo mengine yatatimizwa.

Bwana haishii kwenye unyenyekevu tu bali anafikia upeo wa ukamilifu wake kwa kuinuliwa juu msalabani kwa ajili ya wengi na wanavutwa kwake. Hapa kuna fundisho zito kabisa, yakwamba kazi yoyote ya kitume tuifanyayo lazima iende mpaka upeo wake yaani itoe sifa kamili kwa Mungu. Tuaalikwa kuinuliwa juu mpaka msalabani kama Kristu masiha alivyoinuliwa akitimiza mapenzi ya Baba yake. Kuinuliwa juu ndio wito wa kwaresima, ndio wito wa kubadili maisha ya ndani na kuelekea utakatifu.

Mpendwa, ninakuomba daima ukumbuke kuwa imani si lelemama bali ni shughuli iliyo na madai mpaka kuinuliwa msalabani. Ndiyo kusema tunadaiwa imani ili mapenzi ya Mungu yafanyike daima katika maisha yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari imekuja kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.