2015-03-23 16:59:00

Nyenzo za kufanyia kazi katika maisha na utume wa Kanisa!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo! Tukiwa ndani ya kipindi cha Kwaresma ambapo sote tunaalikwa kujitafiti, kujitathimini na kujiunda upya katika utu wema na haki, tuendelee kutumia nyenzo na misaada tunayopewa na mama Kanisa ili kuweza kutimiza adhma hiyo. Tunapiga mbio katika maisha yetu ya wongofu kwa msaada wa Maandiko Matakatifu, sala, matendo ya upendo na huruma, na pia kwa msaada mkubwa wa mafundisho mbalimbali ya Kanisa. Mama Kanisa anajua njaa na kiu ya watoto wake. Ni kwa mantiki hiyo daima anatupatia lishe stahiki kwa wakati, kwa ajili ya kutusaidia katika safari yetu ya hapa duniani. Mwaliko kwako msikilizaji, tusome ujumbe wa Kwaresma kutoka kwa Viongozi wetu wa Kanisa, humo kuna chakula bora cha kiroho na kijamii.

Tutakumbuka kwamba katika vipindi vilivyopita tulitazama kwa uchache yale yaliyojiri katika Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican, na tukahimizana sana kufahamu yale tuliyoelekezwa na Mtaguso huo Mkuu ili tuweze kufikiri na Kanisa na kwenda pamoja. Na baada ya kuzipitia hati zote 16 za Mtaguso, katika kipindi kilichopita tulianza kuzitazama nyenzo za utekelezaji wa yale ambayo tumejipangia kwa njia ya Mtaguso ule. Tuliziona nyenzo nne ambazo ni, Imani ya kweli, Usikivu, Ujasiri na bidii ya daima.

Mantiki yetu mpendwa Msikilizaji ni hii: Maendeleo yoyote ya kiroho au kimwili hutokana na mipango makini na utejelezaji makini wa mipango hiyo. Endapo katika maisha ukiwa tu mhodari wa kupanga mipango na kuiandika kwa maneno mazuri ajabu, halafu ukakosa kujibidisha katika kuitekeleza, hakika daima utafanana na muota ndoto nzuri na baadaye anabaki tu kutegemea ndoto zake. Katika maisha, tupange mipango kwa umakini, na tuitekeleze tena kwa nyenzo sahihi na ndani ya wakati, ili tusiwe na mipango ya milele. Baada ya kuzitazama nyenzo zile nne, leo mpendwa msikilizaji, tunaendelea na nyenzo nyinginezo, tega sikio vizuri.

Nyenzo ya tano ni Ukweli  katika uwazi. Mpendwa msikilizaji, katika maisha ya kila siku, unaalikwa kujitahidi kuyafahamu yale yanayokuhusu katika ukweli na uwazi wote. Kila mtu kwa maisha yake binafsi au kwa maisha yake ya huduma kwa jamii, anayo mambo ya msingi ambayo ni lazima ayafahamu vizuri ili aweze kuratibisha maisha yake vizuri. Taaluma zote za maisha zinatudai  kufahamu vizuri taaluma hizo ili tuweze kuhudumia watu vizuri. Hali kadhalika katika maisha yetu ya imani, endapo mimi ni Mkristo, ni wajibu wangu msingi kufahamu misingi ya imani yangu, ili niweze kuiishi vema.

Ndipo twasema sasa, sisi tulio waana wa Kanisa ni wajibu wetu kujua ukweli juu ya Mungu na ukweli juu ya Kanisa, ili tupate kujua nafasi yetu na kuwajibika kwetu katika kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani kwa njia ya Kanisa. Mara nyingi waamini wamekuwa baridi katika kuwajibika ndani ya kanisa, pamoja na sababu nyingine nyingi na halali, sababu mmojawapo ni kutokufahamu ukweli juu ya wajibu na nafasi yao, na pengine mambo mengi kutokuwa wazi kwao, ili kutoa nafasi kwa kila mwamini kuona fursa ili kuchangia katika kuziendeleza na kuona pia udhaifu ili kuchangia katika kuboresha. Ieleweke kwamba ni wajibu wa kila mwamini kujibidisha katika ukweli kujua wajibu wake. Hati za mtaguso Mkuu zipo wazi mbele yetu, ni juu yetu sisi kujibidisha kupata ujumbe wake. Wenye wajibu wa kuziweka wazi hati hizo kwa waamini na wafanye hivyo, na waamini kwa upande wao wajibishe daima kutafuta malisho ya majani mabichi ndani ya Kanisa.

Nyenzo ya sita ni Utayari wa kuacha ukale. Mpendwa msikilizaji, Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani, ulileta mambo mengi sana mapya ambayo kwa namna fulani yalileta mtikisiko wa kawaida wa kuweza kuwapanga abiria vizuri. Hii ni hali ya kawaida kabisa katika maisha, kila jambo jipya liwe binafsi au la kifamilia au la kijamii, huleta mtikisiko fulani, uwe ni chanya au hasi, kwa wote au kwa baadhi tu. Mtikisiko ni lazima. Hatuwezi kuwa na Mtaguso Mkuu kama ule, halafu kila mtu akabaki tu vile vile kana kwamba hakuna kilichofanyika. Mtaguso Mkuu ulilenga kuleta mabadiliko, kuingiza hewa mpya ndani ya Kanisa. Mabadiliko hayo ni pamoja na namna zetu za kufikiri na kutenda. Sio wote walibaki salama katika mabadiliko hayo.

Wapo ambao hupenda sana kuishi kwa falsafa ya ‘sisi zamani’! Kila jambo rejea yake ni ‘sisi zamani tulikuwa’. Mtu wa namna hiyo amefungamana na ukale kiasi kwamnba hawezi kuona chema chochote katika usasa, na watu wa sasa hawawezi kufanya jema lolote. Yeye daima maisha ni zamani, mazuri yalikuwepo zamani, watu waadilifu walikuwepo zamani, imani ya kweli ilikuwepo zamani, mapadre wazuri ni wale wa zamani, walimu wazuri ni wale wa zamani...yeye ni zamani na zamani na yeye. Mtu mwenye kichwa cha aina hiyo, huona usasa na maendeleo kuwa ni  dhambi, anasa na starehe. Yeye ni ‘Mr. Sisi zamani’!

Ni falsafa hii ya ya uzamani inawafanya baadhi ya watu washindwe kufanya mabadiliko katika maisha yao binafsi au katika maisha ya kijamii. Mawazo yao hayapo tayari kukaribisha mawazo mapya. Na ndipo utaona watapenda kufanya mambo kizamanizamani, bila kujali hasara au kituko wanacholeta katika jamii wanamoishi. Kwa baadhi ya watu wenye falsafa tete za kizamani, hadi leo hawajapokea Maagizo ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani, na hawajatekeleza hata yodi moja, kwa sababu wao bado wanaamini ile mitaguso ya zamani tu. Wameung’ang’ania ukale na hawapo tayari kuusadaka uzamanizamani wao. Na hiyo tabia za kung’ang’ania uzamani huwa kama ugonjwa wa kuambukiza vile. Utaona mtu wa miaka 30, ana itikadi zote za Mtaguso wa Trento, na anapinga kila kitu cha sasa. Anaamini zaidi katika mifumo waliyoiishi watu zamani, haoni thamani katika maisha ya sasa. Hiyo ni hatari. Hatukatai, katika uzamani, kuna hazina kubwa ya mema, basi tuyachukue hayo, tuchanganye na mapya, ili Kanisa la Mungu lisonge mbele na imani yetu izidi kuwa hai daima.

Kuna falsafa pia isemayo, mazoea yana tabia ya kutokukubali mabadiliko mapema. Hiyo ni hali ya kawaida kabisa ya mwanadamu. Watu ambao mmezoeana sana, inakuwa vigumu kuachana. Kiongozi ambaye mmemzoea sana, inakuwa ngumu sana kuacha falsafa zake. Mambo ambayo umeyazoea sana, inakuwa ngumu kuyaacha mara moja, hali kadhalika mifumo ambayo umeizoea sana, inakuwa ngumu kuibadilisha upesi. Na hali hii hujitokeza kwa rika na kada zote za watu. Sasa hapa fundisho ni hili, tukitaka maendeleo katika maisha, tuwe tayari kupokea mabadiliko kwa kuyasadaka mazoea. Mazoea tu peke yake yanatabia ya kudumaza uwezo wa kufikiri. Mara nyingi tumekosa kupokea hata mafundisho ya mama Kanisa kwa sababu tu ya mazoea fulani. Tukiwa tayari kuyasadaka mazoea, hapo tunajifungulia milango ya maendeleo zaidi ya kiroho na kimwili. Lakini yote yafanywe katika ukweli, uwazi na  nia njema inayoongozwa na hekima ya Kimungu.

Nyenzo ya sita ni Ushirikiano na mshikamano kama wanafamilia ya Mungu. Mpendwa Msikilizaji, baadhi ya mambo ambayo Kanisa limetufundisha kwa njia ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani, ni uelewa juu ya Kanisa. Pamoja na tafanusi nyingine nyingi juu ya Kanisa, tunafundishwa kuwa  Kanisa ni  familia ya Mungu. Tunu mmoja ya maisha ya kifamilia ni upendo unaomwilishwa katika ushirikiano na mshikamano wa kweli. Hali kadhalika sisi katika Kanisa letu kama familia ya Mungu, tunahitaji mshikamano wa kweli kati  yetu na ushirikiano chanya, ili tuweze kujijenga vema kwa msaada wa mafundisho tunayopewa. Wapo ambao kwa akili zembe wanadhani wajibu wa kuendeleza Kanisa ni wa maaskofu na mapadre na watawa. Na kwa aina hiyo ya fikra, utakuta lawama zote zinaelekezwa kwa askofu au kwa paroko au kwa watawa wa siku hizi. Si kweli! Ni wajibu wetu sisi sote, Amka tushirikiane kaza mwende twende pamoja, ili tuliendeleze Kanisa la Mungu lisonge mbele na sisi tuokolewe.

Basi mpendwa msikilizaji tukiwa ndani ya kwaresma ambapo pia twajipima na kujitathimini juu wa uwajibikaji wetu ndani ya Kanisa, jiulize swali, pamoja na mambo mengine mengi ufanyayo ya mfungo, Kwaresma hii unafanya jambo gani la pekee kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa lako?  Tafakari, chukua hatua, kwaresma hii tenda jambo la kishindo kwa ajili ya Kanisa lako. Asante kwa kusikiliza radio Vatican.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican ni Mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.