2015-03-23 16:48:00

Mwilisheni mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo. Tunakukaribisha katika kipindi chetu pendevu cha Kanisa la nyumbani ambamo kwa wakati uliopita tulijaribu kuelezana juu ya nyenzo za kuyamwilisha mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican. Na kwa kipindi hiki tunafunga mjadala kuhusu Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican, kwangu, kwako na kwake, linabaki utekelezaji makini, hasa wakati huu tunapongojea kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, kama kilele cha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Katika kipindi hiki, tunatoa neno la jumla linalikujia mpendwa msikilizaji. Kwanza kabisa, tukumbuke daima sisi binadamu ni viumbe jamii, tunaofanana katika baadhi ya mambo lakini pia tunatofautiana sana katika mambo mengi. Historia zetu ni tofauti, misimamo yetu ni tofauti, itikadi zetu ni tofauti, mielekeo yetu pia ni tofauti na hata matarajio yetu ni tofauti na hivyo tabia zetu kwa ujumla ni tofauti.

Huwa inatokea mara nyingi katika ujamii wetu, kutokana na utofauti huo mambo yakawa hayaendi kabisa, hata kama tupo katika  muungano wa ndoa, au tupo katika familia mmoja, au tupo katika ofisi mmoja an tunafanya shghuli yoyote ile ya pamoja. Tunapoona mambo hayaendi hata kama kwa nje kunaonekana hakuna tatizo, Mtaguso huu umetufundisha, tuketi, tujitathimini, tuone ni nini tunaweza na kwa nini tunaweza, ili tuongeze juhudi na maarifa zaidi; lakini pia tuone ni wapi tunashindwa na kwa nini tunashindwa, ili tujikosoe, tuanze upya tusonge mbele.

Kama tulivyowahi kusema, Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican, haukuitishwa kwa sababu kulikuwa na matatizo mazito kama ilivyokuwa kwa mitaguso mingi iliyopia, hasha. Bali Kanisa lilitaka kujitathimini, kufungua madirisha ili hewa mpya iingie, ili liimarike zaidi na zaidi. Ndivyo nasi waana Kanisa na watu wote tunavyopaswa kufanya.

Endapo wanandoa hawana tabia ya kuketi, kujitathimini, kuulizana kwa upole, kujibu maswali kwa hekima na upole, kwa kweli wanasababisha uvundo mkubwa katika maisha yao ya ndoa, ambapo kunajengeka hali ya kutoaminiana, kuhisiana vibaya daima na hata kutakiana mabaya. Mwenzi anasikia jambo la mwenziwe mtaani, yeye analiamini hivyohivyo na bila hata kuuliza, analivimbishia sura maisha yote. Maandiko Matakatifu yanatufundisha, Umesikia jambo juu ya jirani yako, muulize pengine hakutenda. Na kama alitenda, hatalitenda tena (Ybs 19:13-17). Ukibaki tu kuamini mitaa, utakosa usingizi bila sababu.

Katika familia zetu, tuketi pamoja na watoto wetu, tutathimini maendeleo ya familia yetu. Watoto washirikishwe pia mipango ya maendeleo ya familia. Hakika huweza kutokea mtoto akatoa wazo jema ambalo wote mtashangaa, hekima hiyo kaipata wapi! Si vema watoto wanashtukia tu mambo yanatendeka kimazingaombwezingaombwe, mara fuso linaletwa, mara jengo linajengwa, mara mali zinauzwa. Ushirikishwaji wa watoto katika mipango ya familia inawajengea dhana imara ya kuwajibika na kuhusika zaidi katika familia. Wakuwa wazalendo kweli wa familia.

Katika maofisi yetu, tufanyapo kazi pamoja, vikao halali na vya wazi ni dawa nzuri ya kutibu majungu na malalamiko yasio ya kiima wala kiarifu. Ofisi isiyojua kujitathimini, hufuga wapiga majungu wengi na wazushi  kila mmoja anafanya jitihada ya kumtafuna na kummaliza mwenzake. Na uongozi ukiwa na tabia ya kuendekeza majungu, yaani kufanyia kazi majungu ya mtaani badala ya kuwa na vikao, ofisi hiyo itaharibu kazi na itaharibu afya za watu pia.

Utashangaa ofisi fulani wamejaa wagonjwa watupu tena wana ugonjwa unaofanana, kila siku ruhusa ya kwenda kupumzika. Ukiangalia kwa miwani nyeusi utakuta, watu hao wamejeruhiwa mno na bosi wao kwa msaada wa wapiga majungu. Mkuu wa ofisi naye anakosa ujasiri wa kumhoji mpiga majungu, yeye anakuwa na kichwa chepesi kuamini na kufanyia kazi kila anachokisikia, na mkono mwepesi kuandika yahusu uhamisho. Ofisi isiyojitathimini kwa njia ya vikao halali, itajaa uhamisho bubu mwingi sana. Dawa ni nini? Vikao halali na wazi, vyenye lengo la kujenga. Na katika vikao, tuongee kwa adabu,  tuwe na nidhamu ya kusikilizana na kuelewana vema, sio kukomoana kwa kuraruana kwa maneno ya hovyo na kauli mkuki. Tukifanya hivyo ofisi yetu itasonga mbele na hata sisi wenyewe tutakuwa na afya nzuri.

Mpendwa msikilizaji kwa kipindi kijacho tutaanza kutazama katika hazina yetu. Hivyo jina la Kipindi chetu litakuwa ni  Hazina yetu! Tutaipitia Mafundisho tanzu ya Kanisa, yatakayotusindikiza katika maisha yetu, tayari kujisadaka kwa ajili ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa wale wanaotuzunguka.

Kukumbusha tu mpendwa msikilizaji, usisahau kusoma ujumbe wa Kwaresma kutoka kwa Maaskofu wetu. Zingatia kwa makini pia nyaraka zinazotujia kipindi hiki kutoka kwa Maaskofu wetu. Amka, tushikane mikono, tazama mbele, tufikiri na Kanisa, twende pamoja!

Nikikutakia heri na baraka tele kwa kipindi hiki cha Kwaresma, kutoka katika Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Pambo Martini Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.