2015-03-23 10:17:00

Mshikamano na wakristo wanaoteseka huko Mashariki ya Kati


Askofu mkuu Cyril Vasil, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki pamoja na ujumbe wake, wamerejea tena mjini Vatican baada ya kuhitimisha hija ya kitume kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Syria. Lengo lilikuwa ni kuihakikishia Familia ya Mungu nchini humo, uwepo endelevu wa Baba Mtakatifu Francisko katika shida na mahangaiko yao.

Waamini kamwe wasidhani kwamba, Kanisa limewasahau, bali linaendelea kusali na kuwaombea, pamoja na kuwasaidia kadiri ya uwezo wake, daima likiwa na matumaini kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kutekeleza dhamana na wajibu wake, ili kweli amani, maridhiano na umoja viweze kutawala tena mioyoni mwa wananchi wa Ukanda wa Mashariki ya Kati.

Hii ni changamoto ya kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; mambo yanayomwilishwa katika mchakato wa mshikamano wa udugu na upendo, kwa kusaidiana kwa hali na mali. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kwa niaba ya Baba Mtakatifu, linaendelea kuwaimarisha waamini huko Mashariki ya kati, hususan katika kipindi hiki kigumu katika maisha na historia yao, kwani wanakabiliwa na vita, nyanyaso na dhuluma zinazofanywa kwa misingi ya misimamo mikali ya kidini.

Katika mazingira kama haya, Wakristo wengi wanajikuta wakikata tamaa na hatimaye, kuingia kishawishi cha kuikimbia nchi yao, jambo ambalo ni hatari na linaendelea kusababisha mateso na mahangaiko makubwa kati ya watu.

Askofu mkuu Cyril Vasil anasema, amekutana na watu wakiwa wamegubikwa na shida, mahangaiko na mateso makubwa, lakini pia watu walioonesha imani,  matumaini na furaha hata katika mahangaiko yote haya. Wakristo wanaendelea kusaidiana na kushirikishana hata kile kidogo walichonacho; kwa kuwahudumia majeruhi na kuwazika wafu wao.

Ni Jumuiya ambayo inaguswa mno na mshikamano na uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha yao kana kwamba, anayo majibu yote ya matatizo na mahangaiko yao. Kwa hakika ni watu ambao wanaliona Kanisa kuwa karibu nao zaidi. Wakristo huko Mashariki ya Kati wanaendeleza majadiliano ya kiekumene yanayomikwa katika damu ya mashahidi wa imani, wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni majadiliano yanayosimikwa katika sala na uhalisia wa maisha ya kila siku.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.