2015-03-23 12:17:00

Huruma ya Mungu na haki ni chanda na pete


Mahali panapo kosekana huruma ya Mungu, ni vigumu sana kuweza kupata haki, kama inavyojionesha katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumatatu tarehe 23 Machi 2015, pale mwanamke asiyekuwa na hatia anahukumiwa adhabu ya kifo; mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi anapelekwa mbele ya Yesu, ili apewe adhabu na mwanamke mjane na maskini! Mababa wa Kanisa wanapotafakari sehemu hizi za Neno la Mungu wanalitambua Kanisa kuwa ni: Takatifu, Kanisa linaloogelea katika dimbwi la dhambi na Kanisa maskini na hitaji.

 

Mafarisayo na wakuu wa Makuhani waliomkamata mwanamke mzinzi, walikuwa ni wanafiki na wala rushwa, waliokuwa wanajineemesha kwa udhaifu wa wadhambi kwa kujishikamanisha na Sheria ya Musa na kusahau kwamba, hawakuwa na chembe ya utakatifu wa maisha. Hata wazee wa baraza waliotoa hukumu kwa Suzana mwanamke asiyekuwa na hatia, walikuwa ni wala rushwa wakubwa, lakini kwa nje walijifanya kuwa ni watetezi wa haki.

 

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican siku ya Jumatatu, tarehe 23 Machi 2015. Anasema, rushwa na ufisadi vinawafanya watu kutoonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

 

Hata leo hii, kuna watu ambao wanakosa haki zao msingi kutokana na uwepo wa rushwa, changamoto ya kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuweza kuwaonjesha wengine: matumaini, huruma na mapendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Viongozi wakatili ni wagumu kutoa huruma ya Mungu, lakini wanapaswa kujifunza kutoka kwa Yesu ambaye hakuja kuhukumu bali kutoa maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia kwa wengi.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.