2015-03-21 12:04:00

Waridi lipo kati kati ya miiba!


Tumeingia katika juma la tano la kipindi cha Kwaresma ambapo tunaelekea kuhitimisha safari yetu hii ya toba, safari ya kuukarabati mwenendo wetu mbele ya Mungu na hatimaye tusherehekee kwa mastahili fumbo la ukombozi wetu, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hakika ni safari ambayo si ya lelemama hata kidogo, ni safari iliyojaa changamoto nyingi, safari iliyojaa upinzani mwingi kwani adui yetu shetani naye kamwe hatuachi, anatupigania kwa makusudi ya kuendelea kutufanya kuwa wateja wake wa kudumu.

Dhamira ya dominika hii ya leo inajikita katika kutafakari Fumbo la Msalaba kama kielelezo na dira yetu katika kuelekea kuuona utukufu wa Mungu. Katika desturi ya tangu kale ya Kanisa Katoliki dominika hii ya ya tano huitwa dominika ya kwanza ya mateso. Ni dominika inayotuingiza katika tafakari ya mateso ya Kristo kama kielelezo na nguvu wakati wa safari yetu hii ya toba wakati tukitazamia kuuona utukufu wa Mungu. Hiyo ndiyo kiu na hamu yetu katika kipindi hiki, kutafuta kumuona Kristo, kuutafuta utukufu wa Mungu.

 

Dominika iliyopita tulipokea ujumbe wa matumaini, ujumbe wa furaha, ujumbe ambao ulitutia nguvu ya kuendelea kutembea katika safari hii ya toba. Maneno ya mwanzo katika liturujia ya Misa yalitualika yakisema “Furahi, Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao; furahini ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake”. Ujumbe huu ulitupatia ahadi ya faraja itokayo juu, ahadi ambayo inapatikana pale tu tunaponendelea kumpenda Mungu na kumfanya kuwa ngao yetu. Mzaburi anatuambia kwamba “heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake … sheria ya Bwana ndiyo impendezayo na sheria yake uitafakari mchana na usiku”.

 

Hamu yetu kubwa ni kutaka kumwona Bwana kama wayunani wawili tunaowasikia katika Injili ya dominika hii. Bila shaka tunasimama mbele ya wenzetu na kutaka kuuona huo utukufu wake. Jibu la Kristo kwa wayunai wale ni kwamba “nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu”. Huu ni mwaliko wa kujivua maelekeo na tamaa za ulimwengu huu na kujivika mavazi ya wokovu. Ni mwaliko wa kutoka katika kuyatazama na kuyachuchumilia yaliyo ya chini na kuutazama utukufu wa Mungu katika Msalaba.

 

Ukitaka kuchuma ua la waridi sharti uwe tayari kuchomwa na miiba yake. Uzuri wa utukufu wa Mungu, furaha ya kumwona Mungu ni kujikatalia furaha, starehe na anasa za ulimwengu huu wa leo. “Yeye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele”. Shule ya msalabani inatupatia fundisho moja kubwa ambalo kwalo ndilo tunaweza kuuona utukufu wa Mungu. Fundisho hilo ni: “Baba, ikiwa ni mapenzi yako uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke”. Msalaba wa Kristo ni kilele cha utii kwa sauti ya Mungu, mwanzo wa kumfanya mwenyezi Mungu kuwa Bwana wa maisha ya mwanadamu na kwa utii huo tutamtukuza Mungu.

 

Katika safari yetu hii ya Kwaresma bila shaka tumekutana na vikwazo vingi na pengine kukiona kipindi hiki kuwa mzigo mkubwa sana. Ni kweli ulimwengu na mambo yake unatuvuta, starehe zake zinazidi kuwekewa nakshi nzuri, wapambe wake wanatafuta maneno matamu ya kutuvutia kwake, inachosha, na wakati mwingine tunashawishika kupindisha kidogo. Somo la kwanza la Dominika hii linatuonya katika jambo moja muhimu la kuzingatiwa katika safari hii.

 

Hatutaweza kutembea peke yetu katika hali yetu ya kibinadamu iliyojeruhiwa na dhambi isipokuwa tu pale tutakapojivika utu mpya. Mwenyezi Mungu anaweka ahadi ya kutuumba upya na kuweka roho yake ndani mwetu kwa njia ya sheria zake. Hivyo ni wajibu wetu kuisikiliza sauti hiyo iliyofichika ndani mwetu na kutembea katika njia yake. Zaidi ya yote somo hili la kwanza linatudai kuwa na utayari katika safari hii, mwenyezi Mungu anatuita katika uhuru wetu na si kwamba anatushurutisha kwa kutushika mkono.

 

Maamuzi haya binafsi yanatutaka kwanza kujifunza na kuutambua ukuu wa Mungu. Ndiyo maana katika kipindi hiki tunaalikwa kuwa katika hali ya sala na tafakari ya kina, tukijiweka chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu na kuisikiliza sauti yake. Sauti yake tunaisikia katika Neno lake kupitia masomo mmbalimbali ya Biblia na maandiko ya mababa wa kale. Hivyo, utayari wetu wa kutembea katika safari hii usindikizwa na paji la utii na unyenyekevu mbele ya Mungu. Kristo aliye kielelezo chetu, tunaambiwa katika somo la pili, katika hali ya ubinadamu wake alijitoa kwake Yeye aliye asili ya mema yote kwa sala na maombi na zaidi alijifunza katika hali ya mateso ambayo yalimpata.

 

Hatuwezi kuutambua ukuu wa Mungu katika hali ya kutaka kujitukuza sisi wenyewe na kujitutumua mbele za watu. Hatuwezi kumwona Mungu na utukufu wake tunapokosa kuwa watii na wanyenyekevu mbele yake. Tutambue kwamba mitambo inayoacha kufuata kanuni za uundwaji wake hupoteza hali ya kukamilisha majukumu yake na kuishia kuwa kama “chuma chakavu”. Binadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mungu wetu ni Upendo na kwa upendo wake huo ametufanya nasi kuwa ushuhuda wa mapendo yake. Utukufu wa Mungu unaonekana pale tunapokuwa tayari kuwa mapendo katikati ya wenzetu. Utukufu wa Mungu umesimikwa tayari ndani mwetu kwa njia ya Roho mtakatifu aliyemiminwa katika miyo yetu.

 

Je, tunataka kweli kumuona Yesu? Basi turejee katika uhalisia wetu, tuitambue thamani yetu sisi wanadamu kwamba tumeumbwa kwa sura na mfano wa mwenyezi Mungu. Tushuhudie kwa Upendo wetu wa kikristo. Upendo wetu kwa jirani zetu hasa wale ambao ni wahitaji kabisa, wale wanaoteseka, wale waliodharaurika na hata wale wanaotengwa na ulimwengu huu ndiyo njia ya kutufunulia sura ya Mungu. Tumtafute Kristo katika kupenda kwetu. Huku ndiko pekee utukufu wa Mungu unatung’aria. Tuendelee kutembea katika safari yetu hii ya toba tukimtukuza Mungu na kumtazama katika msalaba. Tusisahau ya kwamba “Waridi hupatikana katikati ya miiba”.

 

TUMSIFU YESU KRISTO

Na Padre Joseph Mosha

Jimbo kuu la Dar es Salaam.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.