2015-03-21 15:44:00

Mnong'ono kati ya wazee!


Wazee wakitaka kuteta jambo wanajitenga kando mahali pa faragha na kunong’ona. Mara nyingi wazee hao wanateta jambo la hekima. Leo tutamwona mzee mmoja tena Rabi (Jalimu) aitwaye Nikodem mwenye jambo zito moyoni anaondoka usiku kwa siri anakwenda kuteta jambo na Rabi Yesu. Maana ya Nikodem ni “ushindi wa Taifa.”

 

Kutokana na matendo yake, yaonekana Nikodem alikuwa mtu mnyofu, mwenye kujiamini sana na mwenye kupenda kuhoji jambo moyoni mwake. Hakuwa jasiri kuonesha waziwazi dukuduku zake hususani zile zinazopingana na rai ya wengi, kwa sababu aliogopa macho ya watu. Lakini apatapo fursa ya faragha ya kuteta na mtu wa kueleweka hapo atatoa rai zake na kutetea fikra zake ili kupata kinaganaga cha mambo.

 

Nikodemu anatupata fundisho la kujihoji mioyoni mwetu endapo tunaona mbele yetu mwanga wa ukweli mpya tunaotakiwa kuupokea, lakini tunajisikia vigumu kuachana na fikra na matendo yetu ya awali, au tunaogopa kukemea uovu utendekao katika kanisa au hata mmomonyoko wa maadili serikalini.

 

Yaonekana Nikodemu alikuwa amefuatilia vya kutosha nyendo za Yesu hivyo anapokutana naye tu anavunja ukimya na kumuweka sawa Yesu: “Rabi sisi tunajua ya kuwa u Rabi (mwalimu) umetoka kwa Mungu.” Kisha anamtolea hoja ya kuthibitisha tamko lake “kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.” (Yoh. 3:2). Ukweli wa mambo Nikodemu hakuwa ameshuhudia ishara yoyote ile aliyoifanya Yesu, kwa sababu ishara ya kwanza ya kugeuza maji kuwa divai Yesu aliifanya Kana, kaskazini - Galilea. Sanasana alichofanya Yesu alipofika Yerusalemu - Yudea ni kuingia Hekaluni na kuwatimua wafanya biashara.

 

Nikodemu alikuwa ameshuhudia vurumai hizo alizofanya Yesu akabaki kushangaa ushujaa huo wa Yesu kwa vile hakutokea kumwona nabii yeyote aliyewahi kufanya jambo la mtindo huo kabla ingawaje alijua hali mbaya iliyokuwa inaendelea mle hekaluni. Nikodemu akawa katika vurugu la akili na kujiuliza peke yake “hivi huyu ni nani mwenye kuthubutu kufanya kitendo cha kijasiri kama hiki hata cha kutumia nguvu kukemea vitendo vya kunajisi hekalu?” Hiyo ndiyo ilikuwa hoja iliyompa Nikodemu mshawasha wa kutaka kumwona mtu huyu asiyetaka unafiki wowote katika mahusiano na Mungu.

 

Yesu anamkatiza Nikodemu na kuanza kuongea jambo jipya kabisa anaposema: “Inabidi kuzaliwa upya.” Kwa hiyo mazungumzo yote ya Injili ya leo yamejengwa juu ya wazo kuu la “kuzaliwa upya.” Uzao wa watu katika ulimwengu huu ni wa kibidamu yaani ni wa kibaolojia. Kumbe,  yabidi kuzaliwa kwa maji na roho ili kuingia katika ulimwengu wa uzao wa kimungu, kwa vile kizaliwacho na mwili ni mwili, na kizaliwacho kwa roho ni roho. Ukiuelewa uwili huo wa uzao ndipo utaweza kufuatilia na kukielewa anachotaka kukisema Yesu katika mazungumzo yale ya faragha.

 

Hebu fuatilia anavyosema Yesu: “Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa.” Lugha hiyo ya Yesu inatupeleka jangwani, Musa alikotengeneza nyoka wa shaba na kumtundika mtini. Kila aliyeumwa na nyoka mwenye sumu kali amwangaliapo nyoka yule wa shaba alipona mara moja. Kwa hiyo neno hili kuinuliwa ni muhimu sana katika Injili ya Yohane. Lakini jinsi tunavyoelewa sisi kibinadamu, “Kuinuliwa” maana yake ni kupandishwa daraja katika maisha, kuwa na cheo, kuwekwa pahala pa juu na kupewa hadhi, heshima na kushabikiwa.

 

Kumbe, ukiangalia kwa jicho la kiroho huko kuinuliwa Msalabani kunamhusu yule mtumishi anayemsema Isaya, yaani mtu wa huzuni, mwanakondoo apelekwaye machinjoni. “Kuinuliwa” huko anakosema Nabii Isaya kulimhusu Masiha ajaye kuwa atainuliwa, na kiti chake cha enzi kitakuwa msalaba.  Mtumishi huyo  siyo mwingine bali ni Yesu Kristo. Kisha Yesu anaendelea kusema: “Ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.”  – Kigiriki neno uzima wa milele ni “Zoen aionion” maana yake “ni sasa,” yaani, Yesu anaposema “zawadi ya uzima wa milele” hamaanishi zawadi ya wakati ujao, la hasha bali ni mang’amuzi ya sasa. Hasemi “atakuwa na uzima wa milele hapo baadaye” bali “anao uzima wa milele”. Kwa hiyo ili kuwa na maisha hayo yabidi kuamini juu ya kuinuliwa kwake juu ya msalaba. Huo ndiyo uzao wa juu, yaani kumwamini yule aliyeinuliwa, kuamini kule kutoa kwake kwa maisha yake na katika utukufu wa Msalaba.

 

Ujumbe wa Yesu kwetu leo ni dhahiri, kwani tunayo tayari mang’amuzi ya Kipasaka. Tunaweza kuelewa kirahisi tofauti ya kuinuliwa kadiri ya kigezo cha ulimwengu huu, na kuinuliwa kule kadiri ya kigezo cha Mungu. Watu wengine wanaona kule kuinuliwa kwa Yesu ni kushindwa. Kumbe mwinjili anaona kuwa ni ujumbe mkuu wa upendo wa Mungu. Kwa hiyo Msalaba hauwi tena ishara ya uchungu na maumivu bali ni ishara ya upendo  “Mungu aliupenda sana ulimwengu huu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

 

Tunaweza sasa kujenga taswira ya maumivu ya kuumwa na nyoka, lakini nyoka huyo ni halisi naye anamaanisha majivuno, makuu, ukandamizaji, uonezi, vita, kuonekana wa juu, kuheshimika na wote kushabikiwa. Ili kupona kutoka na sumu ya kuumwa na nyoka aina hiyo ni kuinua macho na kumwangalia yeye aliyeinuliwa msalabani.

 

Yesu anaendeleza wazo hilo “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.” Huyo Mungu hakumtuma Mwanae duniani ili kuuhukumu bali kuukomboa. Ulimwengu unahukumiwa na msalaba wa Kristu maana yake, hasa pale tunapoishi katika ulimwengu wa ubinafsi, kila mmoja anapojifikiria juu ya mwenyewe tu binafsi, yaani tunapodhani kwamba maisha hayo ndiyo yenyewe mwisho.

 

Kumbe, Msalaba huo wa maisha ndiyo utakaotakasa ubinafsi wetu unaotuzuia kuwa binadamu halisi, na kutufanya kuuacha udhihirike upendo wa Mungu ulio ndani mwetu. Pendekezo hilo jipya litokalo juu, ndiyo mwanga yaani mwanga umefika duniani na kumbe binadamu amependa giza. Kila wakati katika maisha yetu tunaposhawishiwa kujifungia katika giza la ubinafsi wetu, tunaalikwa kuinua macho yetu na kumwangalia Yesu aliyeinuliwa msalabani, yeye anatupa mwanga wa maisha.

 

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB. 








All the contents on this site are copyrighted ©.