2015-03-21 15:13:00

Mifumo yote ya utumwa inadhalilisha utu wa binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko ameianza hija yake ya kichungaji Jimbo kuu la Napoli, Jumamosi tarehe 21 Machi 2015, kwa kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari takatifu ya Pompei, Napoli na baadaye ameendelea na hija yake Jimbo kuu la Napoli kwa kukutana na waamini wa mji wa Scampia.

 

Akiwa katika maeneo haya, Baba Mtakatifu anaitaka Familia ya Mungu Jimbo kuu la Napoli kuondokana na mifumo yote ya utumwa mamboleo, uvunjaji wa sheria, rushwa na ufisadi; mambo ambayo yanachafua hali ya mazingira, utu na heshima ya binadamu!

 

Jimbo kuu la Napoli kwa muda wa saa 10 limeshuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kuonesha ile furaha, amani na utulivu, mambo msingi yanayopaswa kutawala katika maisha ya watu. Umati mkubwa wa Familia ya Mungu, wamemiminika kwa wingi kumwona, kumsalimia na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko ambaye wengi wao wamemsikia na kumwona kwenye Televisheni.

 

Baba Mtakatifu anaitaka Familia ya Mungu Jimbo kuu la Napoli kuonesha cheche za matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kujikita katika utawala wa sheria, vinginevyo watajikuta kwamba, wamepokwa matumaini na hivyo kusababisha majanga kwa watu wasiokuwa na hatia. Uvunjifu wa sheria inachafua sifa na maisha ya watu wengi mjini Napoli, hali ambayo inachangia pia kudidimia kwa sekta ya uchumi, ustawi na maendeleo ya wengi.

 

Baba Mtakatifu ameshuhudia pia umati mkubwa kwa wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaojipatia riziki na mahitaji yao msingi Jimbo kuu la Napoli. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, wahamiaji na wageni wanaonekana kuwa kama ni watu wa daraja la pili, watu wasiokuwa na thamani; lakini watu watambue kwamba, hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; waamini watambue kwamba, ni wasafiri bado wako njiani, kuelekea kwenye makao ya uzima wa milele.

 

Kuna idadi kubwa ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa mji wa Napoli, wanaokabiliwa na ukosefu mkubwa wa fursa za ajira! Kwa mtu asiyekuwa na ajira, utu na heshima yake viko rehani anasema Baba Mtakatifu. Hii inatokana na mfumo na sera duni za kiuchumi ambazo hazitoi kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu. Kuna kundi kubwa la watu linaloendelea kunyanyasika na kudhulumiwa kwa kutakiwa kufanya kazi kwa masaa mengi, lakini kwa ujira kiduchu! Watu wanapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na  heshima yao kama binadamu.

 

Baba Mtakatifu anawataka wananchi kuheshimu sheria za nchi, bila utawala wa sheria, kanuni na maadili; rushwa na ufisadi vitatawala maisha ya wengi na matokeo yake ni kutumbukia katika maisha yasiyokuwa na dira wala mwelekeo mzuri. Rushwa na ufisadi ni mambo yanayochafua na kuharibu utu na heshima ya binadamu, kila mtu anapaswa kusimama kidete kupinga kwa matendo vitendo vyote hivi vinavyomdhalilisha binadamu.

 

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, sera makini zinajikita katika misingi ya: udugu na upendo; huduma makini na utawala wa sheria. Matokeo yake jamii inacharuka kwa maendeleo katika medani mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu Francisko alipowasili kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu ameweka shada la maua mbele ya Sanamu ya Bikira Maria, iliyowekwa mahali hapo na Mwenyeheri Bartolo Longo kunako mwaka 1878.

 

Baba Mtakatifu amejiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria katika maisha na utume wake. Amezungumza na wafanyakazi wa kujitolea waliokuwa wamefurika kwa wingi katika eneo hili. Baba Mtakatifu katika sala yake, amemkabidhi Bikira Maria, mateso na mahangaiko ya wanadamu, wanaoendelea kuogelea katika dimbwi la vita, mauaji, dhuluma na nyanyaso. Kuna kundi kubwa la watu wanaoteseka kutokana na baa la umaskini, lakini zaidi na dhambi. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Ibada ya Rozari takatifu ni silaha ya kutafuta amani na msamaha!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.