2015-03-20 15:33:00

Miaka 20 ya Injili ya Uhai


Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa kichungaji, Injili ya Uhai, Evangelium Vitae kwa mkesha na ibada itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko mjini Roma, Jumanne, tarehe 24 Machi 2015, mkesha wa Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari na Malaika Gabrieli kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi.

 

Tukio hili linaandaliwa na Baraza la Kipapa la familia, ili kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa matunda mengi ambayo amelikirimia Kanisa kutokana na maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Mama Kanisa anapenda pia kuwahamasisha watoto wake kujikita katika maisha ya sala yanayomwilishwa katika imani tendaji.

 

Ratiba inaonesha kwamba, maadhimisho haya yataanza kunako majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za Ulaya kwa tafakari mbali mbali kuhusu Injili ya Uhai. Saa 12: 00 waamini watasali Rozari takatifu na saa 1:00 jioni wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia.

 

Hapa Mama Kanisa anapenda kuonesha uhusiano wa dhati uliopo kati ya Fumbo la Maisha na mang'amuzi yanayojikita katika uhalisia wa maisha ya kijamii. Kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai kuna maanisha kushiriki katika ahadi ya Mungu na mwanadamu.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa,C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.