2015-03-20 08:40:00

Magaidi washughulikiwe, majadiliano ya kidini yaendelezwe


Askofu mkuu Ilario Antoniazzi wa Jimbo kuu la Tunisi, Tunisia anasema, Kanisa linapenda kuonesha moyo wa mshikamano na wote walioguswa na shambulizi la kigaidi lililotokea Tunis na kusababisha watu 25 kufariki dunia, wengi wao wakiwa ni wageni. Kati ya watu watano waliofariki dunia kutoka Tunisia, wawili wao ni magaidi. Askofu mkuu Antoniazzi ametumia fursa hii kuwatembelea na kuwafariji watu waliojeruhiwa kutokana na shambulizi hili ambalo limelaaniwa na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa.

 

Askofu mkuu Antoniazzi anasema, kimsingi watu wengi nchini Tunisia wametikiswa na kuguswa na shambulizi hili kwani wao ni wakarimu na wema, ndiyo maana wamejitokeza kwa wingi sehemu mbali mbali nchini humo kupinga vitendo vya kigaidi vinavyolenga kusambaratisha amani, umoja, mshikamano na demokrasia. Wananchi wa Tunisia ni wapenda amani na wasingependa kutumbukizwa katika majanga ya watu kujitakia kwa kukumbatia ubinafsi.

 

Askofu mkuu Antoniazzi anabainisha kwamba, Kanisa halina woga wowote, litaendelea kutekeleza dhamana na utume wake kwa kuzingatia misingi ya haki, amani, ukweli na upatanisho kati ya watu. Kanisa linaitaka Serikali kupambana vikali na watu wote wanaohusika na vitendo vya kigaidi.

 

Kanisa kwa upande wake, litaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni ili kujenga misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Magaidi wanapaswa kushughulikiwa kisheria na kamwe wasipewe nafasi ya kupandikiza mbegu ya vitisho kati ya watu.

 

Vijana wajengewe misingi na kanuni maadili, wasaidiwe kulinda na kuheshimu zawadi ya uhai. Pale ambapo vijana wanakumbwa na giza katika maisha yao ya kimaadili, wanapoteza dira na mwelekeo wa maisha na wanaweza kutumbukizwa kwa urahisi sana katika vitendo  vya kigaidi kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna vijana wengi kutoka Tunisia kutokana na ukata na ugumu wa maisha, wamejikita wanajiunga na vikundi vya kigaidi.

 

Huu ni wakati wa kuonesha ushuhuda wa maisha unaojikita katika tunu msingi za: Kikristo, kiutu na kimaadili, kwa kushikamana na kusaidiana. Majadiliano ya kidini yanamwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa kupendana, kuthaminiana na kusaidiana.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.