2015-03-19 15:33:00

Papa Francisko kurindima kwenye Baraza kuu la UN


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea na kuzungumza na wajumbe wa Umoja wa Mataifa wakati huu, Umoja wa Mataifa unapoadhimisha miaka 70 tangu ulipoanzishwa. Baba Mtakatifu atazungumza na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 25 Septemba 2015, wakati ambapo Umoja wa Mataifa utakuwa unafanya maamuzi muhimu kuhusu maendeleo, mabadiliko ya tabianchi, amani, ustawi na maendeleo ya binadamu.

 

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kwamba, Baba Mtakatifu atazungumza na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa na baadaye atafanya mazungumzo na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na kushiriki mkutano wa Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon ana matumaini makubwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko atasaidia kutoa changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kuongeza juhudi zaidi katika kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa kujikita katika: masuala ya haki jamii, maridhiano na maelewano kati ya Watu wa Mataifa.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.