2015-03-17 12:14:00

Vijana mkimezwa na malimwengu mtakiona cha mtema kuni


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amehitimisha hija ya kitume nchini Bielorussia kwa kufanya mkesha na vijana pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Familia ya Mungu kutoka Bielorussia, Jumapili tarehe 15 Machi 2015 na baadaye kurejea tena mjini Vatican.

 

Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amewataka waamini kujikita katika maisha ya sala na ushuhuda unaojikita katika umoja, udugu na upendo, dhidi ya ubinafsi, chuki na uhasama. Waamini wawe ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa wote wanaowazunguka na kukutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku.

 

Katika Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili tarehe 15 Machi 2015, Kardinali Parolin ameikumbusha Familia ya Mungu jinsi ambavyo Kanisa lilipitia kipindi kigumu, waamini kuteswa na kunyanyasika; Wakleri kufungwa na kuteswa; Makanisa yakaharibiwa katika kampeni ambayo ilitaka kufuta mioyoni mwa waamini ile sura na chapa ya Mungu, lakini bado waamini waliweza kuwa imara na thabiti katika maisha yao. Hii inaonesha kwamba, mchakato wa kutafuta, kujenga na kudumisha uhuru wa binadamu ni mapambano endelevu yanayoimarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake.

 

Waamini wanachangamotishwa na Kardinali Parolin, kujivunia Ukristo wao na kuendelea kushikamana na Kristo pamoja na Kanisa lake hata kama Kanisa lina watoto ambao wanaogelea katika dhambi na mapungufu ya kibinadamu, kwani daima Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwapokea na kuwasindikiza katika hija yao ya maisha ya kiroho.

 

Jumamosi, jioni, tarehe 14 Machi 2015, Kardinali Pietro Parolin aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Watakatifu Simeone na Elena, kwa kuwakumbusha kwamba, Wakristo ni watu wanaotambua na kuonja huruma na upendo wa Mungu unaokomboa, chemchemi ya furaha, imani na matumaini pasi na kukata tamaa. Mashahidi waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake ni mbegu ya matumaini na ujasiri katika imani. Katika shida na mahangaiko yao, Wakristo wawe na ujasiri wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya sakramenti za Kanisa.

 

Kardinali Parolin anawataka vijana kuhakikisha kwamba, wanautumia vyema ujana wao, kwa kuwapenda na kuwathamini wengine; kwa kuwa ni wachamungu daima wakiyakita maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake. Vijana wanachangamotishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, hawamezwi na malimwengu kwa kupenda mno anasa, mali na fedha; mambo ambayo yanaweza kuwatumbukiza katika ubinafsi na upweke hasi, chanzo cha majanga makubwa katika maisha ya ujana. Vijana wawe na ujasiri wa kumchangua Mungu kuwa ni dira na kiongozi wa maisha yao.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.