2015-03-17 15:36:00

Papa kwa Maaskofu: Endeleeni kuwa thabiti katika utumishi wenu


Baba Mtakatifu Francisko, katika kipindi hiki cha Kwaresima, amewaandikia barua ndugu zake  Maaskofu Katoliki wa Nigeria, ambamo ameomba pia wafikishe salaam zake kwa Jumuiya za Kikristo walizopewa  dhamana  katika huduma za kichungaji. Papa ameonyesha  mshikamano  na mawazo yake juu ya  hali ngumu wanazopita, kwa wakati huu. 
Habari kamili 
Katika barua hiyo, Papa amesema, “wakati huu tunapotembea kuelekea ufufuko wa Bwana tukiwa tumeungana pamoja na kanisa  zima, ninapenda kutoa saalam zangu za dhati , kwenu nyote Maaskofu Wakuu na Maaskofu wa Nigeria , na pia nikiwaomba zifikishe kwa  jamii Kikristo mliyokabidhiwa katika huduma ya kichungaji.  Aidha ninapenda kushirikishana nanyi , baadhi ya mawazo  yangu kuhusu hali halisi za sasa  za maisha  katika nchi yenu”. 
Barua ya Papa , imeendelea kuielezea katika mtazamo wa maisha ya kijamii taifa hili la igeria, taifa kubwa kuliko yote barani Afrika , lenye kuwa na raia zaidi ya milioni 160, linalojulikana pia kwa utendaji wake  si barani Afrika tu lakini  duniani kote. Ameonyesha  kutambua  jinsi taifa hilo katika miaka ya hivi karibuni  limeweza kushuhudia ukuaji wa haraka wa uchumi  na pia kwa mara nyingine kujiwasilisha katika jukwaa la kimataifa kama soko la kuvutia , kutokana na  uwepo wa rasilimali   nyingi, na kwa uwezo wake wa kibiashara. Na pia kwa jinsi linavyojitambulisha lenyewe kuwa mtendaji mkuu katika utatuzi wa baadhi ya migogoro  ya kisiasa barani Afrika.
Lakini wakati huohuo, barua ya Papa imeonyesha kujali matatizo makubwa yanayo kabili taifa hilo , ikiwa ni pamoja na aina mpya ya vurugu za kuvuka mipaka na misimamo mkali inayoendeshwa  kikabila, kijamii na kidini, ambamo kwayo Wanigeria wengi wameuawa, kujeruhiwa na kuwa vilema, kutekwa na kupokonywa  kila vitu au si mali tu lakini hata wapendwa  wao,  nchi yao, maisha yao , utu wao na haki zao, kiasi kwamba watu wengi  hawawezi kurudi makwao. Wote sawia Waumini, Wakristo na Waislamu, wanayapita mateso haya makubwa kama matokeo ya wachache wanaodai kuwa watu wa dini zaidi , ambao hulitumia jina la dini vibaya kwa kutengeneza itikadi zao za kidini kwa  maslahi yao kupitia ukandamizaji na vitisho vya kifo.
Katika hali hizo, Papa alipenda kuwahakikishia kwamba yu karibu na Maaskofu na  wale wote wanaoishi mateso na unyanyasaji huo . Na kwamba kila siku anawakumbuka katika sala zake nakwa mara nyingie anapenda kuwatia shime na faraja kwa  maneno  ya kufariji ya Yesu Kristo, yanayopaswa kusikika daima ndani y amoyo wa kila mmoja :"Nawaachieni amani, amani yangu nawapa" (Yoh 14:27).
Amani, Papa ameendelea kusema, si tu kutokuwepo vita au kuwa na  maelewano katika baadhi ya vipengere vya kisiasa, au kutokuwa na  ubabe wa kupindukia. Lakini  watu wanapaswa kutambua kwamba amani, ni  kwa ajili wote, kama  zawadi inayotoka kwa  Yesu Kristo , Mfalme wa amani, anayewafanya wawili kuwa sawa na mtu mmoja Efe. 2:14). Lakini  ameonya kwamba,  ni  tu wale wenye kupokea  amani ya Kristo ndani ya  mioyo  yao na kuihifadhi, kama mwanga wa kuwaongoza katika njia ya maisha,  wanaweza kuwa  wajenzi wa amani (Rej. Mt 5,9.).
Na kwamba amani ni utendaji wa  kila siku, ni kuwa na ujasiri katika kuiishi  halisi ya kukuza maridhiano na ushirikiano kame sehemu ya  uzoefu wa maisha, na kupanua ujenzi wa madaraja ya majadiliano, huduma kwa wanaoishi kwenye mazingira magumu na wanyonge zaidi waliotengwa.  Kwa maneno mengine,  amani ni ujenzi wa utamaduni wa kukutana.
Katika Barua hii, Papa pia alipenda kutoa shukurani zake za  dhati  kwa Maaskofu,  kwa sababu  katikati ya majaribu mengi na mateso, Kanisa nchini  Nigeria, limeendelea kuhudumia kwa  ukarimu, huruma na msamaha. Na hivyo amewakumbuka Mapadre, watawa wake kwa waume, wamisionari na makatekista ambao licha ya kuhatarisha maisha yao, hatelekezi watu wao wanao waongoza  bali huendelea kubaki  imara katika utumishi wao, wakihubiri wema na uaminifu wa Injili.  
Kwao wote , Papa ametoa shukurani zake za dhati na kuonyesha mshikamano wake , na kuwataka wasichoke kutenda mema.  Kwa ajili yao alitolea shukurani kwa Bwana pia kwa watu wengi toka pande mbalimbali za kijamii, kiutamaduni na kidini ambao kwa mapenzi yao na maamuzi yao thabiti, wamesimama imara kupinga kila aina ya ghasia na fujo , na kwa wale wote wenye  kupendelea neema ya usalama na utulivu  kwa ajili ya wote.  
Papa amewataja watu hao kuwa ni  mfano mzuri wenye kutia  nguvu mpya  ya  kusonga mbele katika kushuhudia manufaa ya amani kama Papa Mstaafu  Benedikto wa XVI, alivyoandika katika waraka wa mwisho wa Sinodi kwa ajili ya  Afrika, kwamba, amani ni matokeo ya utendaji wa nguvu ya  Roho Mtakatifu ambayo hubadilisha mioyo ya waathirika na watesaji wao na hivyo kuweza kurejesha udugu" (Africae Munus, 20) .

Kwa maono haya Papa Francisko amewahimiza  ndugu zake Maaskofu wa Nigeria, kudumu katika uvumilivu na bila kukata tamaa, bali wasonga mbele  pamoja katika njia ya amani (rej Lk 1:79.)na katika kuwaongoza  waathirika, kusaidia maskini na kuelimisha vijana ili kwamba wote  wawe wakuzaji wa haki na umoja katika jamii ya Nigeria. . 

Mwisho Papa,  kupitia barua hii kwa Maaskofu , ametoa  baraka zake za Kitume, pia  Mapadre, watawa, wamisionari, makatekista, waamini na wale wanaotesekana kwa imani yao kwa Kristo . Amesema  Ufufuo wa Bwana  na uwe kichocheo cha uongofu, maridhiano na amani kwa watu wote wa Nigeria! Na mwisho kabisa amewakabidhi chini ya maombezi ya Mama  Maria, Malkia wa Afrika. Na ameomba wasimsahau katika sala zao. . 








All the contents on this site are copyrighted ©.