2015-03-17 11:51:00

Kutakana na mwanamke wa shoka katika tasnia ya habari


Mama Mary Ann Walsh ni kati ya wanawake wa shoka ambaye sehemu kubwa ya maisha yake ameyatumia katika tasnia ya habari, kiasi cha kupatiwa tuzo maalum ya Mtakatifu Francisko wa Sales inayotolewa kwa watu waliojipambanua kutokana na huduma yao katika sekta ya mawasiliano ya jamii.

 

Kwa miaka mingi Mama Mary Ann Walsh alikuwa mkurugenzi wa idara ya habari ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani na mwanachama mashuhuri wa Chama cha Habari cha Wakatoliki Marekani, (CPA). Kwa hakika ni mwanamke wa shoka ambaye amejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa katika tasnia ya habari, mfano bora wa kuigwa na wengi, anasema Rob De Francesco, Rais Chama cha habari cha Wakatoliki Marekani ambaye anafafanua kwa nini wameamua kumtuza mama Mary Ann Walsh tuzo hii ya kimataifa.

 

Mama Mary Ann Walsh, Mtawa wa Shirika la Masista wa Huruma nchini Marekani, ni mwanamke wa shoka aliyejizatiti katika tasnia ya habari tangu katika ujana wake, alipoanza kuandika kwenye Gazeti la "The Evangelist" linalomilikiwa na Jimbo Katoliki la Albany, lililoko Jijini New York, Marekani. Baadaye Mama Mary Ann Walsh alitumwa mjini Roma kuwa mwakilishi wa "The Catholic News Service" na baadaye alikuwa ni mwakilishi wa Wakala huu, Washington, DC.

 

Mama Mary Ann Walsh kunako mwaka 1993 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Denver, Marekani, alikuwa ni mkurugenzi wa mawasiliano. Askofu John Charles Wster, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano ya Jamii, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, ndiye anayetegemewa kumpatia tuzo Mama Mary Ann Walsh.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.