2015-03-17 11:41:00

Bara la Afrika linahitaji amani, utulivu na maendeleo


Nchi mbali mbali Barani Afrika zinaadhimisha Jubilee ya zaidi ya miaka 50 tangu zilipojipatia uhuru wa bendera na kwamba, Bara la Afrika limekuwa likiendelea kucharuka katika medani mbali mbali za maisha licha ya matatizo na changamoto zinazolikabili.

 

Kuanzia tarehe 13 hadi 15 Machi 2015 kumefanyika kongamano kuhusu Bara la Afrika, lililoandaliwa na Shirika la Wamissionari wa Comboni, wakati huu wanapojiandaa kuadhimisha Jubilee ya miaka 150 tangu Mtakatifu Daniele Comboni alipobainisha mbinu mkakati wa Uinjilishaji Barani Afrika. Kongamano hili limewashirikisha viongozi wa Kanisa na watu mashuhuri kutoka Italia.

 

Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani amepembua dhamana na mchango wa Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho kama walivyobainisha Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu kutoka Barani Afrika.

 

Baadhi ya wajumbe wamegusia kuhusu kiini cha taalimungu ya kiafrika; mchango wa Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika: mawasiliano jamii katika ustawi wa Familia ya Mungu Barani Afrika. Kongamano hili limefungwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

 

Mtakatifu Daniel Comboni ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika, changamoto na mwaliko kwa wanasiasa, wachumi na viongozi wa Serikali kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika. Viongozi wa Kanisa kwa upande wao, wawe kweli ni sauti ya kinabii; wakarimu na wenye huruma kadiri ya Kristo mchungaji mwema; watu wenye matumaini kwa maendeleo ya watu wao pasi na kujikatia tamaa wanapokumbana na changamoto na matatizo ya maisha. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa na Familia ya Mungu Barani Afrika.

 

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Kardinali Fernando Filoni, wakati wa mahubiri yake kwenye maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu na kwamba, Kanisa Barani Afrika litaendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa upatanisho, haki na amani kama wanavyohimiza Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu wa Afrika na kukaziwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Dhamana ya Afrika, Africae Munus.

 

Kardinali Filoni anasema Bara la Afrika kwa sasa lina madonda makubwa ya vita na kinzani za kijamii; magonjwa, njaa na umaskini wa hali na kipato. Kuna utajiri mkubwa wa rasilimali ambayo inaendelea kuwanufaisha watu wachache kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ubinafsi, rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliitaka Familia ya Mungu Barani Afrika kusimama imara ili kuanza kujikita kikamilifu katika mchakato wa kujiletea maendeleo yake.

 

Miaka 150 ya maisha na utume wa Mtakatifu Daniel Comboni mi mchango mkubwa katika ustawi na maisha ya Kanisa Barani Afrika. Idadi ya waamini na Majimbo imeongezeka maradufu, mchango mkubwa unaotolewa na Familia ya Mungu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Bara la Afrika linahitaji kuoneshwa upendo na mshikamano wa kidugu. Bara la Afrika linahitaji amani, utulivu na maridhiano.

 

Halina haja ya kuona makundi makubwa ya wahamiaji wanaokimbia nchi zao kutokana na vita, njaa na maradhi. Biashara haramu ya silaha na binadamu; utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanadhohofisha ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika. Kardinali Filoni anasema, Kanisa Barani Afrika halina budi kuwekeza kwa Yesu Kristo kama chemchemi ya imani, matumaini, mapendo na mshikamano wa kidugu. Bara la Afrika lisiwe ni kiwazo na pingamizi la maendeleo, bali sehemu ambayo inashiriki kikamilifu katika maendeleo na ustawi wa Jumuiya ya Kimataifa.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.