2015-03-16 10:10:00

Vijana wajibikeni kwa matendo yenu!


 

Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, hivi karibuni ameadhimisha Jubilee ya miaka 25 tangu Kituo cha Vijana Wakatoliki cha Mji wa Furaha kilipoanzishwa, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa vijana wanaojikita katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, kimaadili na utu wema. Huu ni mwaliko kwa vijana kuendelea kuwa kweli ni wajenzi wa haki na amani; umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuendelea kusali kwa ajili ya kuwaombea viongozi wa taifa, ili waweze kutekeleza dhamana na utume wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini Kenya.

Kardinali Njue amewataka vijana kuepuka kishawishi cha kutaka kutafuta mafanikio ya maisha kwa njia za mkato, matokeo yake, wanaweza kujikita wakitumiwa na watu wamabaya, wabinafsi na mafisadi kwa ajili ya mafao ya binafsi. Vijana wametakiwa kuwa imara na thabiti katika maamuzi ya maisha yao; daima wakijitahidi kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu, lakini zaidi kwa kumwilisha Amri za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha. Vijana waoneshe fadhila ya unyenyekevu kwa kumpokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili aweze kuwaonesha njia.

Wakati  huo huo, Askofu mkuu Charles Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan ya Kusini amewakumbusha vijana kwamba, ujana ni mali, lakini fainali ni uzeeni. Amewataka vijana wawe ni tumaini katika kufikiri na kutenda kwao; kwa kujenga na kuimarisha: familia, jamii na nchi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Kamwe vijana wasikate tama katika maisha, kwani daima wanaweza kuwa wema na kufanya mabadiliko katika maisha.

Askofu mkuu Balvo anawataka vijana kusoma kwa umakini mkubwa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwa mwaka 2015 ngazi ya Kijimbo itakayoadhimishwa, Jumapili ya Matawi, unaoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye moyo safi maana watamwona Mungu”. Vijana wanatakiwa kuwa na usafi wa moyo kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wanatakiwa kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mungu katika maisha yao. Vijana watambue kwamba, wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa la leo na kesho na tangu wakati huu wanawajibika kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa. Vijana wajikite katika kumtumikia Mungu, kutenda mema na kuendelea kuwa ni chemchemi ya furaha, maisha na matumaini; mambo yanayosaidia kuleta tofauti katika maisha. Jubilee hii imehudhuriwa na vijana zaidi ya 7, 000 kutoka katika Majimbo 26 yanayounda Kanisa Katoliki Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, kwa msaada wa AMECEA.








All the contents on this site are copyrighted ©.