2015-03-16 11:41:00

Mwenyeheri Oscar Romero


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia ambaye pia alikuwa ni msimamizi mkuu wa mchakato wa kumtangaza Askofu mkuu Oscar Romero aliyeuwa kikatili nchini Salvador kutokana na chuki za imani kunako tarehe 24 Machi 1980 atatangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 23 Mei 2015. Ibada hii inatarajiwa kuongozwa na Kardinali Angelo Amato, Rais wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko. Ibada hii itafanyika San Salvador.

Familia ya Mungu nchini El Salvador inalishukuru Kanisa kwa kutambua na kuthamini mchango wa Askofu mkuu Oscar Romero aliyejisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, changamoto kwa waamini kutafuta na kujikita katika utakatifu wa maisha kwa njia ya ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko kama ilivyokuwa kwa Askofu mkuu Oscar Romero. Askofu mkuu Paglia anabainisha kwamba, baada ya mchakato wa kumtangaza Askofu mkuu Romero kuwa ni mwenyeheri, hatua ya pili ni kuendeleza mchakato utakaomwezesha kutangazwa rasmi kuwa ni Mtakatifu na mfano wa kuigwa na Kanisa zima.

Ushuhuda wake ni chachu ambayo inaendelea kufanyiwa kazi na Familia ya Mungu nchini El Salvador, hasa miongoni mwa maskini, kwani Askofu mkuu Oscar alikuwa ni kiongozi wa watu aliyewapenda kipeo, kiasi hata cha baadhi ya wananchi kumchukia na matokeo yake wakataka kumfuta kutoka katika uso wa dunia, lakini bado anaendelea kuwa ni faraja kwa wengi na mwombezi wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii anasema Askofu mkuu Vincenzo Paglia.

Kila siku kuna umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema wanaotembelea kaburi na Mtumishi wa Mungu Askofu mkuu Oscar Romero, ili kusali na kuomba maombezi yake katika shida na mahangaiko yao ya kiroho na kimwili. Watu hawaogopi tena vita ya wenyewe kwa wenyewe bali adui yao mkubwa kwa sasa ni biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya yanayoendelea kusababisha majanga makubwa miongoni mwa vijana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.