2015-03-16 09:52:00

Mshikamano wa upendo na udugu nchini Malawi


Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi limeanzisha kampeni kubwa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko makubwa yaliyotokea nchini humo hivi karibuni kwa kuchangisha kiasi cha dolla za kimarekani million 2. 2. Kanisa Katoliki nchini Malawi lilikusanya sadaka yote iliyotolewa Kanisani, Jumapili 8 Februari 2015 ili kuwasaidia wananchi walioathirika kutokana na mafuriko nchini humo.

Sadaka ya shukrani kwa ajili ya maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi na nane wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, ilitolewa pia kwa ajili ya nia hii njema. Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, linaishukuru Familia ya Mungu nchini humo kwa kuguswa na mahangaiko ya jirani zao, kiasi cha kuchangia kwa hali na mali, ili kuwasaidia waathirika.

Kwa hakika wanasema Maaskofu, hiki kimekuwa ni kipindi ambacho Familia ya Mungu nchini humo imeonesha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu kwa kuweka kando tofauti zao msingi. Maaskofu wanalishukuru Kanisa la Kiulimwengu kwa kuonesha mshikamano wa kidugu na kwa namna ya pekee, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, imesaidia sana kukusanya msaada kwa ajili ya wananchi wa Malawi, changamoto kwa Familia ya Mungu, kuendelea kuwasaidia wananchi wa Malawi kadiri ya uwezo wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.