2015-03-16 10:19:00

Dumisheni misingi ya haki, amani, upatanisho na demokrasia


Askofu mkuu Gabriel Mbilinyi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe, CEAST anasema kwamba, kwa sasa changamoto kubwa katika nchi hizi ni kuhakikisha kwamba, zinajenga na kuimarisha misingi ya: haki, amani na upatanisho wa kitaifa sanjari na kukuza demokrasia na haki jamii katika medani mbali mbali za maisha. Askofu mkuu Mbilinyi ameyasema haya hivi karibuni wakati wa kufungua mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe huko Luena.

Angola inapojiandaa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 40 tangu ilipojipataia uhuru wake, Maaskofu wanabainisha kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinawaelemea wananchi wengi wa Angola, lakini zaidi ni maskini na vijana wanaoshindwa kupata mahitaji yao msingi. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la bei ya mazao ya chakula; ongezeko la watu wasiokuwa na ajira, hali ambayo inachangia pia vitendo vya uvunjifu wa amani na kwamba, rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni mambo yanayoendelea kuleta changamoto kubwa katika majiundo ya watu kitaaluma, kimaadili na kiroho.

Maaskofu wanasema kuna haja ya kuwalinda, kuwaheshimu na kuwaenzi wanawake, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya jamii kwa kuondokana na mfumo dume ambao kwa sasa umepitwa na wakati. Wanaume na wanawake wanapaswa kushirikiana na kukamilishana kama ulivyo mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Mila na tamaduni zilizopitwa na wakati hazina nafasi tena katika maisha ya wananchi wa Angola.

Maaskofu Katoliki Angola wanaonya kuhusu ongezeko la makundi ya watu wenye misimamo mikali ya kidini wanaotishia usalama na maisha ya watu nchini humo. Mwelekeo wa namna hii unapandikiza mbegu ya chuki, fitina na kisasi kati ya watu.

Maaskofu wanasema kuna haja ya kujenga na kudumisha amani na utulivu, upendo na mshikamano katika maisha ya ndoa na familia, kwa kutambua kwamba, familia ni shule ya haki, amani na utakatifu wa maisha. Maaskofu wameyasema haya kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015.

Baraza la Maaskofu Katoliki Angola linaandaa mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazojikita katika Uinjilishaji mpya, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Parokia kama kitalu cha Uinjilishaji; utekelezaji wake ambao unatarajiwa kufanyika katika kipindi cha mwaka 2016. Maaskofu wanaendelea kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha a utume wake, wakati huu anapokumbuka miaka miwili tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, utume ambao aliuanza rasmi hapo tarehe 19 Machi 2013, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu na msimamizi wa Kanisa zima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.