2015-03-14 15:43:00

Mchakato wa katiba Tanzania una kasoro!


Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu Katiba inayopendekezwa, mahakama ya kadhi na hali ya usalama na amani ya nchi.

Sisi Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania linaloundwa na Taasisi za Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) tuliokutana leo tarehe 10.03.2015, tumepata nafasi ya kujadili kwa kina kuhusu hali ya usalama wa nchi ilivyo sasa na mustakabali wake, Katiba inayopendekezwa na uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi.

 

Baada ya kutafakari yote hayo, Jukwaa limefikia maazimio yafuatayo:

Kuhusu uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi: Suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini kama tulivyotoa maoni yetu kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria (Januari 16, 2015); barua yetu kwa Waziri Mkuu na matamko mbalimbali yaliyokwisha kutolewa kuhusu jambo hili; Mahakama ya Kadhi inakiuka misingi ya Taifa hili kuwa na Serikali isiyokuwa na dini wala mfumo wa sheria unaobagua raia wake kwa misingi ya dini. Pia mjadala unaoendelea unavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 Ibara ya 19.

 

Kwa kuendelea kujadili suala hili katika Ilani za Vyama vya Siasa, Majukwaa ya Kisiasa na Bungeni, limeligawa Taifa letu, Serikali, Bunge, Mahakama na wananchi. Mahakama ya Kadhi imekuwa likiendelea kutumiwa na wanasiasa kama mtaji wao wa kujipatia madaraka kwa gharama za kuleta chuki za kidini. Kwa dhamiri safi, Jukwaa linatamka wazi kuwa mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya masuala hayo bila kuihusisha serikali wala waumini wa dini nyingine.

 

 

Kuhusu Katiba inayopendekezwa: Katiba Inayopendekezwa imeleta mgawanyiko mkubwa katika Taifa kwani imepatikana kwa njia zisizo za kiadilifu; na mchakato wake umeendeshwa kwa hila na ubabe. Aidha, Katiba Inayopendekezwa haijajibu bado matakwa na malalamiko ya wananchi kwenye masuala mbalimbali (Muundo wa serikali, miiko na maadili ya viongozi wa umma, haki za binadamu, madaraka ya Rais, uwiano wa mihimili ya dola n.k).

 

Ikumbukwe Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa ahadi ya Serikali kuipa dini Mahakama ya Kadhi. Inashangaza kuwa hata Serikali inatoa rushwa ili kufikia malengo yake!!! Kwa hali kama hii, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa.

 

Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya HAPANA kwa  Katiba Inayopendekezwa kwa sababu zilizotajwa hapo juu.

 

Hali ya usalama wa nchi ulivyo sasa: Jukwaa linasikitishwa na viashiria pevu vya ugaidi vilivyoanza kujitokeza nchini kwa takribani miaka mitano iliyopita. Kumekuwa na vitendo vinavyoashiria kuchipuka kwa ugaidi kama vile uvamizi wa vituo vya polisi, kuporwa silaha na mauaji ya polisi, mafunzo ya kareti katika nyumba za Ibada, mafunzo ya itikadi kali za kidini kwa watoto (Kilimanjaro), tukio la Amboni Tanga, mauaji ya viongozi wa dini (Buselesele, Zanzibar, Arusha), uchomaji wa nyumba za Ibada na kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa dini.

 

Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino):  Jukwaa linasikitishwa na mwendelezo wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino) na ukatili unaosababisha ulemavu wa kudumu wa maalbino katika nchi yetu. Hali hii inatishia utulivu, amani na umoja wa kitaifa tuliokuwa nao kama taifa la mfano barani Afrika. Jukwaa linawaasa wananchi kuacha tabia hii ya kuua albino. Jukwaa linaamini kuwa kukosekana kwa uwajibikaji wa viongozi wa serikali na kuongezeka kwa wigo wa kipato kati ya walionacho na wasionacho kunachangia ongezeko la vitendo hivyo viovu. Jukwaa linajiuliza: mbona tembo na ng’ombe wakiuawa operesheni maalum zinafanyika na viongozi wanawajibika, kwa nini maalbino wakiuawa viongozi hawawajibiki?

 

Kutokana na hayo yote, Jukwaa linatilia shaka dhamira thabiti ya uongozi wa Chama Tawala na Serikali yake katika kuvitokomeza vitendo vya kigaidi, mauaji ya albino na uvunjifu wa amani unaoendelea hasa kutokana mikakati hafifu na udhaifu mkubwa uliojitokeza wakati wa kuyashughulikia masuala hayo. Kwa kuwa Chama Tawala na Serikali wameshindwa kusimamia misingi iliyolea taifa kama serikali isiyo ya kidini na taifa lenye amani; umoja na utulivu; Jukwaa linawaelekeza waumini wote na wenye mapenzi mema wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao kufanya maamuzi yanayolitanguliza Taifa badala ya kutanguliza mazoea, mapokeo, itikadi na ushabiki wa chama fulani cha Siasa.

 

YATOSHA  KWA SIKU  MAOVU WAKE: MATAYO 6:34








All the contents on this site are copyrighted ©.