2015-03-06 07:55:00

Kipaumbele cha kwanza ni familia


Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linapania kuhakikisha kwamba, mchakato wa shughuli na mikakati ya kiuchungaji na uinjilishaji mpya zinajikita katika mambo makuu matatu: Familia, Parokia na Shule. Ni maneno ya Kardinali Ricardo Blàzquez Pèrez, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Valladolid aliyeteuliwa hivi karibuni na hatimaye, kusimikwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Kardinali wa nne, tangu Kardinali wa kwanza Jimboni humo kutangazwa kunako mwaka 1868. Hili ni tukio ambalo limepokelewa na Familia ya Mungu Jimboni humo kwa moyo wa shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, limesaidia kujenga na kuimarisha mshikamano wa dhati kati ya Askofu na waamini wake.

Utamadunisho ni dhana ambayo inafanyiwa kazi na Maaskofu Katoliki Hispania ili kuhakikisha kwamba, Injili inasafisha na kupyaisha masuala mbali mbali ya tamaduni za watu nchini humo kadiri ya tunu msingi za Kiinjili. Hispania imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa tamaduni, fursa makini kwa Mama Kanisa kuzitumia ili kuwafikishia watu wengi Injili ya Furaha, kwa njia ya sana ana katekesi makini. Matukio mbali mbali ya maisha ya kiroho nchini Hispania ni nafasi ya kukuza na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho kwa kutumia pia njia za mawasiliano ya kijamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania lina mtandao mkubwa wa vyombo vya mawasiliano ya kijamii ambavyo vinaweza kutumiwa katika mchakato wa Uinjilishaji, ingawa bado wananchi wengi hawajawatayari kusikiliza habari zinazorushwa na vyombo vya Kanisa. Hapa Kanisa halina budi kuwahamasisha watu kujenga utamaduni wa kupenda na kuthamini matangazo yanayorushwa na vyombo vya Kanisa kama sehemu ya Uinjilishaji.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maalum ya Maaskofu kuhusu familia pamoja na maandalizi yanayoendelea kwa sasa kwa ajili ya Sinodi ya Maaskofu ni fursa makini ambazo Mama Kanisa anaweza kuzitumia vyema kwa ajili ya kuhamasisha utangazaji wa Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa, licha ya matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazojitokeza. Maaskofu nchini Hispania wanaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utume na maisha ya ndoa na familia. Kumekuwepo na maadhimisho, mikutano, wasraha na makongamano ili kupembua kwa kina na mapana fursa, matatizo na changamoto za maisha ya ndoa na familia.

Maaskofu nchini Hispania wanaendelea kuboresha maandalizi kwa ajili ya wanandoa watarajiwa; wanaimarisha vyama vya utume kwa maisha ya ndoa na familia. Mambo yote haya yanapania kuimaisha imani, matumaini na mapendo katika maisha ya ndoa na familia, ili kukabiliana na changamoto mbali mbali kwa hekima na busara ya Kimungu. Familia ya Mungu nchini Hispania ina matumaini makubwa kwa Sinodi ya Maaskofu itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba, 2015.

Maaskofu wanabainisha kwamba, zawadi ya imani, tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiroho na kimaadili zinarithishwa kwa vijana wa kizazi kipya kwa njia ya: familia, parokia na shule. Watoto hawana budi kusaidiwa kutambua umuhimu wa maisha ya kiroho katika makuzi yao, ili hatimaye, waweze kuwa ni waamini watakaowajibika zaidi katika maisha na utume wao katika medani mbali mbali za kijamii. Familia ya Mungu iwajibike na kujibidisha kurithisha imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni kati ya changamoto kubwa za maisha na utume wa Kanisa nchini Hispania. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Hispania limeendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika wa athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Caritas inasaidia pia familia maskini, kwa kuwajengea uwezo wa kupambana na baa la umaskini; kwa njia ya mshikamano wa upendo katika sekta ya elimu. Maskini ni kati ya amana ya Kanisa na wainjilishaji wakuu, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, wanatambua kwamba, Kanisa linawapenda, linawatetea na kuwahudumia.

Kardinali Riccardo B. Perèz anabainisha kwamba,  kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kidogo la vijana wanaotaka kujiunga na maisha ya kitawa na kipadre. Huu ni muujiza ambao Mwenyezi Mungu anapenda kuitendea Familia ya Mungu nchini Hispania na kwamba, Maaskofu pamoja na wasaidizi wao wanaendelea kuhamasisha miito kwa kutambua kuwa, familia bora zinazalisha waamini wenye imani thabiti, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mwaka wa Watawa Duniani ni fursa makini ya kuhamasisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wenye mashiko na mvuto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.