2015-03-05 14:00:00

Mapambano dhidi ya umaskini!


Wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kila mwaka wanawasili nchini Uingereza ili kutafuta fursa za kazi na wanapofanikiwa kuzipata wanachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji na ustawi wa wananchi wa Uingereza. Hili ni kundi la watu wanaofanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa, ni watu ambao mchango wao umeiwezesha Uingereza kuandika historia tofauti nyakati hizi.

Huu ni mchango wa Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, wakati huu wa maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo tarehe 7 Mei 2015. Wahamiaji ni kati ya mada zinazofanyiwa kazi na wanasiasa wakati huu wanapojinadi ili kutafuta ridhaa kutoka kwa wananchi ili waweze kuongoza. Wahamiaji ni watu wanaosadaka maisha yao ili kutafuta nafuu ya maisha Barani Ulaya. Baadhi yao ni watu ambao wameonja shida ya vita, dhuluma na nyanyaso za kidini.

Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na wapiga kura wanaposikiliza maoni ya wanasiasa wakijinadi ili kuomba kura za wananchi. Wahamiaji ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na vyama vya kisiasa nchini Uingereza kwa kuwaheshimu na kuwathamini wahamiaji na wakimbizi. Utu na heshima yao kama binadamu ni mambo msingi ya kuzingatiwa na kwamba, licha ya mateso na mahangaiko yao, wanachangia kwa kiasi kikubwa ustawi na maendeleo ya Uingereza. Kwa bahati mbaya wahamiaji na wageni wamekuwa wakinyanyaswa na kudhulumiwa haki zao msingi kana kwamba, wao si watu wanaopaswa kuheshimiwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza hivi karibuni katika barua yao ya kichungaji wamewataka waamini na watu wenye mapenzi mema, kuwapatia kura zao viongozi wanaojali utu na heshima ya binadamu; wanaoguswa na umaskini wa watu wao; viongozi wanaotetea na kusimamia kwa vitendo Injili ya Uhai. Maaskofu wanaonya kuhusu dhana ya ubaguzi wa rangi inayoweza kutumiwa na baadhi ya wanasiasa ili kupata ridhaa ya wananchi.

Viongozi wanaowania madaraka waoneshe sera na mikakati itakayowajengea vijana wa kizazi kipya matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Uingereza ni nchi ambayo ina matabaka makubwa ya watu tajiri, lakini kwa upende mwingine kuna watu wanaoteseka kutokana na umaskini. Ongezeko la matabaka kati ya akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi na wale wanaokula na kushiba kiasi cha kukufuru ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya jamii. Ikiwa kama mambo haya hayataweza kushughulikiwa kikamilifu, amani na utulivu vinaweza kutoweka katika jamii.

Kardinali Vincent Nichols anasema kuna haja ya kuwajengea matumaini vijana wa kizazi kipya bila kuwatumbukiza katika dhana ya ubaguzi wa rangi. Vijana wakikosa matumaini, watagubikwa na upweke hasi na matokeo yake ni kuanza kujiunga na makundi ya kigaidi kama inavyojionesha wakati huu. Watu wenye misimamo mikali ya kiimani, kiitikadi na kijamii wasipewe nafasi ya kuvuruga wananchi wa Uingereza, kwani matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.