Wasimamizi wa uchaguzi mkuu nchini Lesotho uliofanyika hivi karibuni kutoka Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA wanasema kwamba, uchaguzi
ulikuwa huru na wa haki na kwamba, watu wengi wametumia haki yao ya kikatiba kutekeleza
wajibu wao barabara katika hali ya amani na utulivu.
Waangalizi wa vituo vya
kupigia kura kutoka kwenye vyama mbali mbali walisimamia zoezi hili kwa ufanisi mkubwa.
Wajumbe kutoka IMBISA walikaribishwa kwa heshima na upendo, kila mahali walipotembelea
ili kukagua zoezi zima la upigaji kura.
Baraza la Maaskofu Katoliki Lesotho
katika barua yake ya kichungaji kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu, liliikumbusha
Familia ya Mungu nchini Lesotho umuhimu wa kuweka mbele mafao ya wengi, umoja na mshikamano
wa kitaifa badala ya kugubikwa na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; mambo ambayo
yamekuwa ni chanzo cha majanga kwa nchi nyingi wakati na baada ya uchaguzi.