2015-03-03 08:56:01

Hata maskini wana haki ya kufaidika na maboresho katika sekta ya afya!


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, watu wanapata tiba na huduma msingi za kijamii bila ubaguzi wala upendeleo, kwani hii ni sehemu ya haki yao msingi. Jitihada za maboresho katika sekta ya afya zinazopania kukinga, kutibu na kuponya magonjwa mbali mbali hazina budi kuendelezwa ili kuwafikia watu wengi zaidi.

Ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao makuu mjini Geneva, Usswis, wakati alipokuwa anachangia mada kwenye Jukwaa la Kijamii la Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu haki msingi za binadamu. Anabainisha kwamba, Kanisa Katoliki ni mdau mkubwa katika utoaji wa huduma kwenye sekta ya afya sehemu mbali mbali za dunia, hususan kwenye maeneo ya vijijini, miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya Serikali zinashindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake kutokana na kizingiti cha haki miliki inayohodhiwa na viwanda vingi vinavyotengeneza dawa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, hali ambayo inaviwezesha kupata faida kubwa kwa gharama ya maisha ya watu. Pili, baadhi ya wawekezaji wanashindwa kuwekeza katika tafiti, huduma na utengenezaji wa dawa ikiwa kama wanaona kwamba, hawatapata faida kubwa. Hii ndiyo hali halisi kwa Jumuiya ya Kimataifa kushindwa kupambana kikamilifu na magonjwa kama: Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na Ebola ambayo imesababisha maafa makubwa kwa wananchi wa Afrika Magharibi. Wawekezaji katika viwanda vya madawa wanatafuta faida kubwa.

Askofu mkuu SIlvano Maria Tomasi anakiri kwamba, watoto ni kundi ambalo halijapewa kipaumbele cha pekee katika mikakati ya utengenezaji wa dawa kwa ajili ya watoto, kiasi cha baadhi ya wazazi kutumia kipimo cha kufikirika ambacho wakati mwingine kinaweza kusababisha madhara. Tatizo kama hili kwa masuala ya Ukimwi, limepewa ufumbuzi, changamoto kwa wadau mbali mbali kuendelea kufanya maboresho katika sekta ya farmasia kwa ajili ya dawa za watoto.

Hati miliki za watengenezaji wa dawa za binadamu ziheshimiwe, lakini pia wamiliki wake waguswe na mahangaiko ya jirani zao, ili kukuza na kuendeleza haki ya kupata huduma bora kutoka katika sekta ya afya jamii, ili kutafuta mafao ya wengi, kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na udugu pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya Uhai, Utu na Heshima ya Binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.