2015-03-02 08:57:44

Vijana ni jeuri ya Kanisa!


Kwa mara ya kwanza Kanisa Katoliki nchini Angola litaadhimisha Siku ya Vijana Kitaifa itakayoanza kutimua vumbi hapo tarege 26 hadi tarehe 30 Agosti 2015, kwa kuwahusisha vijana zaidi elfu tatu kutoka katika Jimbo la Huambo. “vijana ni mashuhuda wa upendo wa Kristo” ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya siku ya kwanza ya vijana kitaifa nchini Angola.

Padre Armando Alberto Pinho, Katibu wa Idara ya utume wa vijana, Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe anasema kwamba, tukio hili litakuwa ni fursa kwa vijana wa Angola kuonja cheche za maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa katika ngazi ya kitaifa. Lengo ni kuamsha, kuchochea na kukoleza upendo wa vijana kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuwasaidia vijana kuonesha na kuchangia nguvu zao katika ustawi na maendeleo ya jamii kwa kuleta mageuzi ya kina katika maisha na vipaumbele vyao.

Maaskofu wa Angola wanapania pia kuwahamasisha vijana ili kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa njia ya maisha ya Kipadre na Kitawa, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko. Katika maadhimisho ya siku ya vijana kitaifa nchini Angola, vijana watajengewa uwezo wa kujikita katika majadiliano katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Ni fursa kwa vijana wa kizazi kipya nchini Angola kukutana na Mwenyezi Mungu katika maisha yao ya ujana kwa njia ya imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.