2015-03-02 09:38:56

Upendo wake watosha!


Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Padre Benno Kikudo kwenye Parokia ya Mavurunza, Jimbo kuu la Dar es Salaam katika maadhimisho ya Jumapili ya pili ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe 1 Machi 2015.
Baba au babu yetu Ibrahim, akitambua kitu kimoja maishani "Katika mlima wa Bwana itapatikana" yaani, "Yehova yire". Mungu hamtupi mja wake. Mungu wetu ni Mungu anayewalisha watu wake asali itokayo mwambani. Ni Mungu anayewalisha waja wake kwa unono wa ngano. Ni Mungu aliyeshusha manna kutoka juu. Ni Mungu aliyemlisha Eliya kwa kinywa cha kunguru na baadaye hata kupitia mjane wa Sarepta (1 Wafalme 17:1 - 16). Mungu wa Ibrahim ni Mungu wetu yaani ni Mungu anayetuwezeshea, "Yehova Yire" maishani mwetu. Mungu huyu anataka nini kutoka kwetu leo ?
- Anahitaji upendo wetu tu, kama upendo mnyoofu wa mzee Ibrahim.
- Mungu anahitaji imani yetu isiyoteteleka, isiyoyoyumbishwa au kujiuliza mara mbili. Kama Ibrahim tuondoke tu.

- Mungu wetu anataka sisi tumvae Kristo kama Paulo wa Somo la pili. Nini kitatutenga na upendo wa Kristo ? (Warumi 8:32). Kwetu kuishi kuwe Kristu tu, na kufa kuwe ni faida. Maisha yetu tusionee fahari cho chote isipokuwa msalaba wa Kristu (Wagalatia 6:14). Tuonje tunapopoteza kwa ajili ya Mungu ndipo tunapopata.
Katika maisha yetu ya kila siku, Mungu anatupitisha katika milima mbali ya mkutano naye. Katika mlima Horebu Musa anakutana na Mungu na kupewa jukumu la kuwatoa wana wa Israeli utumwani (Kutoka 3:1). Ni mlima huu huu pia nabii Eliya anamwendea Mungu baada ya kumkimbia Ahab na mkewe Yezebeli (1Wafalme 19:1 - 18). Mungu anakutana na Musa tena mlima Sinai ili kuchukua amri kumi za Mungu (Kutoka 19:1- 25). Na katika mlimani Nebo (nchini Jordan ya sasa) Musa ataitizama nchi ya ahadi kwa mbali (Yoshua1 -3). Na atakayewavusha wana wa Israeli ni Yoshua.
Katika somo la kwanza leo, Mungu anakutana na Ibrahim katika mlima Moria au Sayuni. Hapa anasikia wito wa Mungu na yu tayari kuutekeleza. Yaani, kumtolea mwanaye wa pekee Isaka sadaka. Mwisho, katika injili yetu ya leo tunasikia juu ya mlima Tabor ambao Yesu anakwea yeye na wafuasi wake watatu - Petro, Yakobo na Yohane (Marko 9:2 - 8). Milima yote yatuambia nini?
Familia zetu ni kama milima midogo midogo. Mungu anaongea nasi kupitia familia zetu kama alivyoongea na Ibrahim. Mungu anataka tumsikie yeye na mwanaye mpendwa Yesu Kristo. Tukimsikia Kristu katika familia zetu - yeye atafanya makao ndani yetu. Na lo lote tumuombalo atatupa. Mungu anafanyika "Yehova Yire" ndani ya familia ye yote inayomsikia na kumpenda. Tumuheshimu Mungu, tumpe nafasi ya kwanza na kubwa katika familia zetu, tutaona daima muujiza huu "katika mlima wa Mungu itapatikana". Tutasomesha, tutalisha, tutavisha watoto wetu kwa vile Mungu hata siku moja hawezi kutupatia ng'e badala ya samaki au jiwe badala ya mkate.
Dunia yetu ina sauti nyingi za marafiki, ndugu na hata wapenzi wetu. Lakini kila uchao tumeonja kusalitiwa nao na kuachwa wapweke. Tunaye mmoja aliyetuita rafiki (Yohana 15:15 - 17). Na huyu ndiye aliyetuambia yote, bila kificho toka kwa baba. Huyu si mwingine, ni Kristo. Paulo katuambia katika somo la pili, upendo wake watosha. Na hakuna kiwezacho kututenga na upendo wake.
Wapendwa, Tuiendee milima ya familia zetu kwa upendo, imani, uelewano na msamaha. Kwa vile milima ya familia imefanyika kwa udongo na mawe ya kiroho. Siku zitakuja, Kristu alimwambia mwanamke Msamaria, ambapo waabuduo kweli, wataabudu kwa roho..(Yohane 4:23).
Nawatakieni Jumapili njema ya Kwaresima.
Padre Benno Michael Kikudo,
Jimbo kuu la Dar Es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.