2015-03-02 08:37:49

Hata Sudan, Wakristo wananyanyaswa!


Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushuhudia dhuluma, nyanyaso na ukatili usiokuwa na kifani dhidi ya Wakristo huko Syria na Iraq, lakini wachunguzi wa mambo ya kidini wanasema kwamba, hata Sudan Kongwe, mambo si shwari kwani hata huko Wakristo wananyanyaswa, wanadhulumiwa na kubaguliwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hivi ni vitendo vinavyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama Sudan Kongwe.

Ni ushuhuda unaotolewa na Mwanasheria Mohamed Mustafa Alnour wakati wa mkutano wa kimataifa uliokuwa unapembua taarifa ya mwaka kutoka kwa wananchi wa Italia nchini Sudan Kongwe. Licha ya katiba ya nchi ya mwaka 2005 inayotoa uhuru wa kuabudu, lakini hautekelezwi kwani hapa kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni “Sharia” ya dini ya Kiislam ambayo ni msingi wa sheria zote za nchi. Itakumbukwa kwamba, wananchi wa Sudan wamegawanyika katika makundi makuu matatu: kuna waamini wa dini ya Kiislam, Wakristo na waamini wa dini nyingine.

Wakristo na waamini wa dini nyingine wanahesabiwa kuwa ni kundi la chini kijamii na kwamba, hawana haki sawa kama waamini wa dini ya Kiislam, hali ambayo inasababisha mpasuko mkubwa kati ya wananchi wa Sudan Kongwe. Tangu baada ya kuitishwa kwa kura ya maoni na hivyo kuanzishwa kwa Jamhuri ya Wananchi wa Sudan ya Kusini, Serikali ya Sudan Kongwe imeanza mchakato wa siri wa kutaka kuyadhibiti Makanisa na kwamba, kwa sasa hakuna ruhusa ya kujenga nyumba mpya za ibada.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.