2015-02-28 12:01:52

Sikiliza kwa makini!


Ndugu msomaji, tunaongozwa katika tafakari hii na vifungu vifuatavyo kutoka katika Maandiko Matakatifu! Unaweza kuanza kwanza kwa kujisomea na baadaye tafakari hii itakusaidia kulifahamu vyema zaidi Neno la Mungu kwa Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka Be wa Kanisa.
    Mwa. 22;1-2,9a, 10-13, 15-18
    Rum. 8;31-34
    Mk. 9; 2-10.


Katika Makanisa ya Bizantina huko Ulaya mashariki, sura ya Kristo huoneshwa kama bwana na mtawala wa muda na wakati wote. Ndiyo tafakari yetu ya leo – sura kamili ya Kristo inawekwa mbele yetu. Sote twajua kuwa maisha ya Kristo ni fumbo. Lakini yeye ametuonesha Mungu na hivyo twaweza kuongea juu ya utukufu wa Mungu uliojionesha kwetu. Hali hii yatuonesha kuwa Yesu alijionesha kwetu na hivyo hakubaki tu fumbo.

Sikia sauti ya Mungu – huyu ndiye mwanangu mpendwa wangu msikilizeni yeye. Hilo fumbo limefunuliwa kwetu. Kwa tamko hili urithi wetu kama wana wa Mungu unawekwa wazi. Leo Mungu ajionesha kwetu. Mt. Yohane wa Msalaba anasema – tangu Baba alipotamka pale mlimani Tabor – huyu ndiye mwananngu mpemdwa msikilizeni yeye, Mungu Baba kwa namna moja alikamilisha ufunuo wake, akabaki bubu. Alisema kila kitu. Hana kitu kingine kipya cha kufunua. Alikamilisha ufunuo wake kwetu.

Alama zilizopo: a. Mlima - mahali pa agano kati ya Mungu na mtu – sasa yaonekana wazi kuwa mlima mpya wa Mungu ni Yesu – Yesu ni mahali pa kukutana kati ya Mungu na watu – siyo tena mlimani. B. Mawingu na kivuli – yaonesha uwepo wa Mungu – mjumber sasa ni Kristo. C. Sauti ya Mungu; huyu ndiye mwanangu – Mungu anajifunua kwetu, na kusema yeye ni nani - sasa tuna dunia mpya, namna mpya ya kuelewa ukweli, namna mpya ya kuishi, namna mpya ya kuishi imani yetu na namna mpya ya kuishi maisha yetu – pamoja na Kristo tunao ufahamu mkubwa kuhusu Mungu. Yesu ndiye sheria mpya, ni juu zaidi ya sheria za mwanadamu na manabii.

Kugeuka sura – ni utangulizi wa Pasaka – tunapoitwa sisi sote katika ushuhuda wa imani yetu ya kila siku – hivyo maisha yetu yahitaji ufunuo wa Mungu hata katika maisha ya kawaida. Kugeuka sura – huangaza matembezi yetu ya imani-mitume waliona utukufu wa Mungu. kwa maisha yetu ya kila siku – wengine wanaweza kuuona utukufu wa Mungu?

Kugeuka sura – huangaza pia maisha yetu ya zamani –mazuri na mabaya – yale mazuri yanaendelezwa na mabaya yanaachwa. Neno la Mungu leo hii – lazima lituvuruge katika imani yetu – kile kilichodhaniwa kuwa fumbo sasa si fumbo tena kwa maana ya kuwa Mungu yu pamoja nasi na ameonekana kwetu na ametuambia wazi kile tutakiwacho kufanya. Hakika imani yahitaji kusaidiwa na matokeo hai – leo tunapata bahati hiyo. Ni msukumo na changamoto kwetu sisi kuishi kama watu wa mwanga na si wa giza tena. Tumgeukie Mungu mwanga wa kweli ili atuangaze na atuongoze. Je, nasi tumegeuka sura zetu au tumebaki hivyo hata baada ya kukutana na Mungu?

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.