2015-02-28 13:44:00

Jengeni utandawazi wa mshikamano!


Maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Shirikisho la vyama vya ushirika nchini Italia ni sehemu ya mchango uliotolewa na Kanisa nchini Italia na ni mkakati wa kupambana na ukosefu wa fursa za ajira na athari katika maisha ya kijamii; na huu ukawa ni mwanzo wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu yanayojikita katika mshikamano unaoongozwa na kanuni auni. Huu ni utajiri mkubwa unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa kama alivyobainisha Papa Leo wa kumi na tatu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 28 Februari 2015 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la vyama vya ushirika nchini Italia kwa kuwataka kuangalia mbele kwa imani na matumaini; kwa kuwajibika sanjari na kuibua vyama vya ushirika, ili kupambana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mateso na mahangaiko ya watu kutokana na sera na mikakati potofu ya masuala ya uchumi na fedha.

Utandawazi usiojali utu na heshima ya binadamu umepelekea kuibuka kwa wimbi kubwa la watu wasiokuwa na ajira, umaskini wa hali na kipato; utu na heshima ya mwanadamu vimewekwa rehani badala ya utandawazi kukoleza mshikamano kama alivyotamani kuona Papa Leo wa kumi na tatu. Hii inapaswa kuwa ni changamoto endelevu kwa vyama vya ushirika kuhakikisha kwamba, vinashirikisha: uzoefu, mbinu na mafanikio ili kujenga matumaini mapya katika mifumo ya kiuchumi inayokatisha tamaa.

Wanachama wa vyama vya ushirika waendelee kuwa ni Manabii kwa kuzingatia tunu msingi za kimaadili na utu wema. Wasaidie kufufua na kuendeleza sekta ya kilimo; wawekeze katika ujenzi wa makazi ya watu pamoja na kutoa mikopo nafuu itakayowasaidia watu kujikwamua na athari za myumbo wa uchumi kimataifa kwa kuzingatia mambo makuu yafuatayo:

Kwanza kabisa, Baba Mtakatifu anavihamasisha vyama vya ushirika kuwa ni chachu ya maendeleo miongoni mwa maskini, ili kutengeneza fursa za ajira kwa wasiokuwa na kazi, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vijana wa kizazi kipya, kwani ukosefu wa ajira unavuruga matumaini yao bila kusahau kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi pamoja na kuokoa makampuni yanayokufa na hivyo kusababisha hasara kubwa katika jamii.

Pili, Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa vyama vya ushirika kuwekeza katika sekta ya huduma ya afya na jamii, kwani kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha na kushuka kwa hali ya maisha, kuna kundi kubwa la watu ambalo halina uwezo wa kugharimia huduma za afya ya jamii. Kwa kuwekeza katika huduma kama hii ni mchakato wa kumwilisha upendo kati ya watu na kuwatuliza; hii ndiyo kanuni ya auni kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Huu unaweza kuwa ni mnyororo wa upendo na mshikamano na Kanisa katika utoaji wa huduma, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu!

Tatu, Baba Mtakatifu anasema, sera na mikakati ya kiuchumi haina budi kusaidia mchakato wa kuendeleza haki jamii, utu na heshima ya binadamu, ili kujenga na kuimarisha uwajibikaji wa kijamii badala ya mtindo wa sasa wa kujielekeza katika soko kwa kujikita katika ubinafsi na faida kubwa: mchakato wa uzalishaji na huduma uwahusishe watu wengi zaidi, hiki ndicho kiini cha vyama vya ushirika katika asili ya mzizi neno!

Nne, Baba Mtakatifu Francisko anawashauri wanaushirika kuwekeza zaidi katika ustawi na maendeleo ya familia; kwa kufanya mlingano sawia kati ya kazi na familia; wanawake wapewe fursa ya kutekeleza wajibu na dhamana yao ya kimama pamoja na kukuza karama na vipaji vyao, lengo ni kuendeleza mafao ya wengi kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao, kwa kuweka pamoja rasilimali na kuonesha uwezo wa kuitekeleza nia hii njema katika matendo. Kwa njia hii, utu na heshima ya binadamu vtadumishwa na kuendelezwa; amani na utulivu vitashamiri ndani ya jamii pamoja na kuendelea kuwekeza zaidi.

Fedha na mali visiwafanye watu kuwa watumwa wa Shetani, kwani hapa ndio mwanzo mwa majanga kwa binadamu. Fedha isaidie kumhudumia mwanadamu katika ukweli na haki, ili kujenga uchumi unaosimikwa katika ukweli kwa ajili ya mafao ya wengi. Vyama vya ushirika vijitanue zaidi na zaidi kwa kushikamana na vyama vingine ili kupata mwelekeo wa kimataifa. Huu ni mwaliko anasema Baba Mtakatifu Francisko kushirikiana kwa karibu zaidi na Parokia pamoja na Majimbo yao; kwa kuheshimu karama na tofauti zilizopo, lakini daima kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.