2015-02-28 08:41:20

Boko Haram na utandawazi vinatishia familia nchini Nigeria


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linabainisha kwamba, Familia ni shule ya kwanza ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni; ni Kanisa dogo la nyumbani; mahali ambapo waamini wanajifunza: utakatifu, upendo na msamaha wa kweli. Lakini familia nchini Nigeria zinakabiliana na changamoto nyingi na kati ya hizi ni kwamba, familia nyingi zimemezwa mno na malimwengu na kwamba, mfungamano wa maisha na tunu bora za kifamilia unavurugwa na mashambulizi ya mara kwa mara yanyofanywa na Kikundi cha Boko Haram, ambacho kwa sasa ni tishio la maisha, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, athari za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknojia zinajionesha kwa namna ya pekee nchini Nigeria. Matumizi ya mitandao ya kijamii ambayo kimsingi ilipaswa kuwaunganisha watu kwa sasa inaonekana kuwa ni kati ya "majanga" ya kifamilia, kwani matumizi mabaya ya mitandao yamepelekea uaminifu na udumifu katika maisha ya ndoa na familia kulega lega, kiasi kwamba, ndoa nyingi zinaendelea kuvunjika. Maaskofu wanawahimiza wanafamilia kuwa na matumizi bora na sahihi ya mitandao ya kijamii.

Mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko Haram yanaendelea kupandikiza mbegu ya: kifo, chuki na uhasama kati ya wananchi wa Nigeria. Mashambulizi haya pamoja na homa ya uchaguzi mkuu nchini humo ni kati ya mambo ambayo kwa sasa yanazikosesha familia nyingi amani na utulivu wa ndani. Watu wengi wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na mashambulizi haya kiasi cha kuwakatisha watu tamaa! Kuna wanawake na wasichana wanatekwa na kunyanyaswa kijinsia; mambo yote haya yanadhalilisha utu na heshima ya wananchi wa Nigeria. Kutokana na kuhofia usalama wa maisha, kuna kundi kubwa la watoto ambalo limepotezana na wazazi pamoja na walezi wao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linalaani sana vitendo vya Kikundi cha Boko Haram kuwatumia watoto kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kuwafungia mabomu ya kujilipua. Huu ni unyama wa hali ya juu kabisa ambao kamwe hauwezi kuvumiliwa. Baadhi ya wanasiasa uchwara na waliofilisika kwa kumezwa mno na uchu wa mali na madaraka, wamekuwa wakiwatumia vijana nchini Nigeria kufanya vurugu na kuvunja amani; mambo ambayo yanabomoa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kiasi cha kuwafanya vijana wengi kukosa dira na mwelekeo wa maisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linaiomba Serikali pamoja na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatoa uhuru na usalama kwa familia ili ziweze kutekeleza dhamana na utume wake kwa kuwapatia watoto malezi na elimu bora itakayowasaidia kupambana na maisha kwa sasa na kwa siku za usoni. Vita na kinzani za kijamii ni mambo ambayo hayana budi kudhibitiwa, ili haki, amani na maridhiano yaweze kutawala tena nchini Nigeria.







All the contents on this site are copyrighted ©.