2015-02-27 09:10:34

Zingatieni kanuni maadili katika masuala ya fedha!


Viongozi wa Mfuko wa "Centesimus Annus" kwa ajili ya Baba Mtakatifu, Alhamisi tarehe 26 Februari 2015 wamewasilisha tuzo ya pili kwa washindi wa awamu ya pili ya Mfuko huu ambao wamejipambanua kwa kuzingatia kanuni maadili katika masuala ya uchumi na maendeleo ya kijamii mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hili ndilo lengo kuu lililomsukuma Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1993 kuanzisha Mfuko wa "Centesimus Annus", ili kusaidia kuyatakatifuza malimwengu kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili kama anavyokazia Bwana Domino Sugranyes Bickel, Rais wa Mfuko huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Bwana Bickel amefafanua kwa kina na mapana mchakato wa mageuzi ya kiuchumi katika sekta ya fedha na maendeleo ya jamii kwa kukazia kanuni maadili. Lengo ni kupambana na: rushwa pamoja na ufisadi sanjari na kuwalinda walaji ambao kwa sasa wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani, kimsingi yanalenga kufanya maboresho katika masuala ya uchumi na maendeleo ya watu, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu; kurekebisha mifumo ambayo imepelekea kuanguka kwa uchumi wa kimataifa kwa miaka ya hivi karibuni. Soko halina budi kujikita katika huduma kwa jamii na wala si vinginevyo.

Mfuko huu unapenda pia kuwahamasisha wasomi na wachumi kujikita katika kanuni maadili wanapotekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya jamii, ili kweli uchumi uwe ni kwa ajili ya mafao na ustawi wa jamii. Katika miaka ya hivi karibuni, wachumi wengi wamejikuta wakiwa ni watumwa wa soko la fedha kimataifa, kiasi cha kutengeneza jangwa linalowatenga watu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko na badala yake, uchumi usaidie mchakato wa ujenzi wa utandawazi unaojikita katika mshikamano wa upendo na udugu, kwa kujali mateso na mahangaiko ya watu wa kawaida kabisa ndani ya jamii.

Monsinyo Antonio Scotti, mjumbe wa tuzo ya Mfuko wa Centesimus Annus anasema kwamba, changamoto ya ujenzi wa utandawazi unoajali na kuguswa na mahangaiko ya wengi bado haujagusa mioyo ya watu wengi. Sera na mikakati mingi ya uchumi bado haojatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu na matokeo yake, binadamu amekuwa kama chombo cha kuzalisha utajiri lakini anaishia kutengwa na mifumo ya uchumi kimataifa. Kanisa linapenda kuunga mkono sera na mikakati ya kiuchumi inayojikita katika mshikamano wa udugu unaoongozwa na kanuni ya auni.

Professa Michael Konrad, Katibu mkuu wa tuzo ya Mfuko wa Centesimus Annus anasema kwamba, wametambua mchango ambao umetolewa na Pierre Lauzun kutoka Ufaransa katika kukuza na kudumisha sera na mikakati ya uchumi inayoguswa na mahangaiki ya watu na ndiyo maana ametunukiwa tuzo ya pili ya Mfuko wa Centesimus Annus kwa mwaka 2015. Ni mchumi ambaye anafafanua kwa kina na mapana jinsi ambavyo Jamii inaweza kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Soko la bidhaa na huduma halina budi kuwa na sheria na kanuni zinazoongoza kwa kujikita katika maadili na utu wema, ili kuwa na uhuru mpana zaidi. Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa asili ni sayansi inayolenga kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mafao ya wengi kama anavyopambanua Bwana Arturo Bellocq Montano kutoka Uruguay. Kwa upande wake Bwana Alexander Stunmvoll kutoka Australia anafafanua kwamba, Mafundisho Jamii ya Kanisa yana utajiri mkubwa katika mchakato wa kukuza na kudumisha mahusiano ya kimataifa.

Bwana Sugranyes Bickel anahitimisha mazungumzo ya viongozi wakuu wa Mfuko wa Centesimus Annus kwa kukazia changamoto zinazobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume: Injili ya Furaha "Evengalii gaudium" kwa kukazia kanuni msingi za maisha ya Kiinjili kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na wala si fedha wala faida kubwa. Taasisi za fedha na uchumi hazina budi kufanya marekebisho makubwa kwa kujikita katika kanuni maadili zinazomwilishwa katika medani mbali mbali za maisha na kwamba, hapa kuna fursa tele, watu wakipania wanaweza kutekeleza dhamana hii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.