Yaliyojiri wakati wa ziara ya Rais Kikwete, nchini Zambia
Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu amesema kuwa nafasi ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika maendeleo
ya Tanzania na amani ya Bara la Afrika ni mambo yasiyotiliwa shaka tena, akitamani
naye apate mafanikio kama Rais Kikwete. Aidha, Rais Lungu amesema kuwa Rais Kikwete
ameonyesha kiwango kikubwa na cha juu cha uongozi, ambacho kinathibitishwa na aina
ya mafanikio ambayo ameyaleta katika miaka yote ya uongozi wake.
Rais Lungu
alifagilia na kusisitiza mafanikio hayo ya Rais Kikwete na uongozi wake kwa nyakati
mbili tofauti, Jumatano, Februari 25, 2015, katika siku ya kwanza ya ziara rasmi ya
siku mbili ya Rais Kikwete nchini Zambia kwa mwaliko wa Rais Lungu. “Nina mengi ya
kujifunza kutoka kwa Mheshimiwa Kikwete ambaye kama mnavyojua anajiandaa kumaliza
muda wake wa uongozi. Mimi bado mpya kabisa katika uongozi wa juu na hivyo nina mengi
ya kujifunza kutoka kwake kwa sababu amefanikiwa sana katika uongozi wa nchi yake,
“ Rais Lungu aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliohudhuriwa na Rais Kikwete
baada ya viongozi hao wawili kumaliza mazungumzo rasmi kati yao.
Akizungumza
wakati wa dhifa ya taifa ambayo Rais Lungu alimwandalia Rais Kikwete kwenye Hoteli
ya Taj Pamodzi mjini Lusaka, Rais Lungu alirudia kumpongeza na kumsifia Rais Kikwete
kwa uongozi bora. “Umeonyesha uongozi wa kutukuka sana ambao unathibitishwa na mafanikio
makubwa katika miaka yote ya urais wako. Umeimarisha, umesimamia na kudumisha utawala
bora, umepanua sana uhuru wa kila aina katika Tanzania ukiwemo uhuru wa vyombo vya
habari. Tunakupongeza kwa mafanikio hayo na baadhi yetu tunaoanza uongozi tunatamani
sana kufuata nyayo zao,” alisema Rais Lungu na kuongeza:
“Mchango wako katika
kusaka amani katika Bara la Afrika ni jambo la kupongezwa sana na ni chimbuko la heshima
kwetu sote na kwa Bara letu lote. Mchango wako katika maendeleo ya Tanzania na Bara
la Afrika ni mambo yasiyotiliwa shaka na yoyote. Ni matumaini yangu na nataka kufuata
nyayo za uongozi wako.”
Wakati wa dhifa hiyo, Baba wa Taifa la Zambia, Mzee
Kenneth Kaunda alikunwa mno na muziki wa Malaika uliokuwa unatumbuizwa na bendi moja
kiasi cha kuingia uwanjani na kumkaribisha Rais Kikwete pamoja na Rais Lungu uwanjani
na kwa pamoja wakasakata rumba. Rais Kikwete ambaye alikuwa Zambia kwa ziara rasmi
kutokana na mwaliko wa Rais Lungu anakuwa kiongozi wa kwanza wa nje kutembelea Zambia
rasmi tokea Rais Lungu ashike madaraka ya kuongoza Zambia mwezi uliopita.
Wakati
huo huo, Zambia imeomba Tanzania kuiuzia nchi hiyo ya jirani gesi asilia kwa
madhumuni ya kuzalisha umeme na kupanua wigo wa uzalishaji wa viwandani. Aidha, Tanzania
na Zambia zimekubaliana kuifufua Reli ya TAZARA kati ya nchi hizo mbili kwa kukabiliana
ipasavyo na changamoto na matatizo ambayo kwa muda sasa yamekuwa yanakwamisha utendaji
bora wa reli hiyo iliyojengwa kwa nia ya kuiwezesha Zambia kupata njia ya kufikia
baharini kwa urahisi zaidi na kusafirisha bidhaa zake kwenda nje.
Ombi hilo
na makubaliano kuhusu TAZARA yalifikiwa, Jumatano, Februari 25, 2015 wakati wa mazungumzo
rasmi kati ya nchi hizo mbili ikiwa ni sehemu ya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku
mbili iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete katika Zambia kwa mwaliko wa Rais Edgar Chagwa Lungu. Mazungumzo hayo yalifanyika
Ikulu ya Zambia, mjini Lusaka.
Katika mazungumzo hayo yaliyochukua muda mrefu,
Rais Kikwete na Rais Lungu waliongoza nchi zao katika majadiliano kuhusu masuala mbali
mbali ikiwa ni pamoja na ombi la Zambia kutaka kununua gesi kutoka Tanzania na jinsi
ya kufufua Reli ya TAZARA. Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Lungu alimwomba Rais Kikwete
akubali Tanzania iuzie gesi asilia Zambia, ombi ambalo Rais Kikwete alilikubali bila
kusita.
“Hakuna shaka kuwa tuko tayari kuwauzieni gesi asilia ndugu zetu wa
Zambia. Linalohitajika ni kwa Zambia kuweza kujenga bomba la kusafirishia gesi hiyo
kutoka Tanzania hadi Zambia. Mwambie yoyote ambaye anaweza kutoa mkopo wa ujenzi wa
bomba la kusafirisha gesi kuwa Tanzania iko tayari kuwauzieni gesi,”alisema Rais Kikwete
wakati wa mazungumzo hayo.
Kuhusu ufufuaji wa Reli ya TAZARA, viongozi hao
wawili walikubaliana kuangalia changamoto za kiuongozi na utendaji, changamoto za
kiufundi, changamoto za kisheria na changamoto za kimuundo, ambazo zinakwamisha uendeshaji
wa ufanisi wa Reli hiyo. Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,600 inaunganisha Dar
es Salaam na Kapiri Mposhi, Zambia, ilijengwa kwa mkopo wa dola za Marekani milioni
500 kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni
mwa miaka 1970.
Hata hivyo, Reli hiyo ilikabiliwa na changamoto kiasi cha kwamba
sasa inachukua muda wa siku 12 kwa treni kusafiri kati ya vituo hivyo viwili vikuu
wakati inachukua kiasi cha siku tano tu kwa magari kusafiri kati ya Dar es Salaam
na Kapiri Mposhi. Aidha, Reli hiyo yenye uwezo wa kubeba mizigo tani milioni tano
za mizigo, mwaka 2014, ilibeba mizigo yenye uzito wa tani 280,000 tu. Serikali ya
China imekubali kimsingi kusaidia kuifufua Reli hiyo lakini baada ya kupokelewa kwa
ripoti ya uchunguzi unaofanywa kuhusu chanzo na ukubwa wa matatizo yanayoikabili Reli
hiyo.
Rais Kikwete akutana kwa kifungua kinywa na Mzee Kaunda, KK!
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Alhamis asubuhi,
Februari 26, 2015, amekutana kwa kifungua kinywa na Mwanzilishi wa Taifa la Zambia
na Rais wa Kwanza wa nchi hiyo, Mheshimiwa Kenneth David Kaunda. Aidha, Rais Kikwete
ambaye amemaliza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika Zambia, ameweka shada
la maua kwenye kaburi la Mama Betty Muntikhe Kaunda, hayati mke wa Mzee Kaunda.
Rais
Kikwete ambaye amekuwa kiongozi wa kwanza wa nje kualikwa kutembelea Zambia kwa ziara
rasmi tokea Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu kushika madaraka
ya kuongoza nchi hiyo mwezi uliopita, amewasili nyumbani kwa Mzee Kaunda katika eneo
la State Lodge Area, Leopards Hill, kiasi cha kilomita 26 kutoka mjini Lusaka, kiasi
cha saa mbili na dakika 40 asubuhi.
Rais Kikwete na ujumbe wake wa watu wachache
amelakiwa na Bwana Kaweche Kaunda, mmoja wa watoto wa Mzee Kaunda ambaye amemwongoza
hadi kwenye kaburi la mama yake, Betty Kaunda, ambako Rais Kikwete ameweka shada la
maua. Rais Kikwete amekaribishwa nyumbani kwa Mzee Kaunda na Mzee mwenyewe ambaye
kama ilivyo jadi yake alikuwa ameshikilia kitambaa cheupe mkononi.
Baada ya
kuweka saini kwenye kitabu cha wageni, Mzee Kaunda na Rais Kikwete walianza mazungumzo
wakati wa kifungua kinywa na kwa saa mbili walizungumzia mambo mengi, hasa yale ya
kijamii bila kuingiza siasa sana. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na watoto wawili
wa Mzee Kaunda, Bwana Kaweche Kaunda wa kiume na Bibi Cheswa Kaunda Silwizya ambaye
ni mtoto wa mwisho wa Mzee Kaunda na Hayati Betty Kaunda. Aidha, mazungumzo hayo yalihudhuriwa
na Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Balozi wa Zambia nchini Tanzania.
Rais
Kikwete amemwambia Mzee Kaunda: “Wewe ni mmoja wa mashujaa wetu katika Bara la Afrika.
Mzee Kaunda wewe ni nyota wa Bara letu, ambaye umehamasisha na kuwatia moyo watu wengi
kukabiliana na changamoto za maendeleo. Tunakushukuru sana kwa mchango wako katika
maendeleo ya Bara letu na tutaendelea kukuenzi kwa mchango huu. Tunakutakia maisha
marefu na afya njema sana.”
Rais Kaunda amemwambia Rais Kikwete kuwa nyumba
hiyo ambayo anaishi kwa sasa iliyoko katika mazingira yenye mandhari ya kuvutia ya
misitu ilijengwa kwa ajili yake na Rais wa tatu wa Zambia, Hayati Levy Mwanawasa.
“Nyumba hii nilijengewa na Serikali ya Rais Mwanawasa.” “Rais Mwanawasa alifanya jambo
zuri, muhimu na la wajibu kabisa kwa sababu unastahili nyumba yenye hadhi ya namna
hii kwa mchango wako kwa wananchi wa Zambia na Afrika katika maisha yako,” Rais Kikwete
amemjibu Mzee Kaunda.
Rais Kikwete alipotaka kujua siri ya afya yake nzuri
kwa umri wake mkubwa, Mzee Kaunda ambaye anafikisha umri wa miaka 91 katika miezi
miwili ijayo, amemjibu: “vegetarian life” akiwa na maana ya kuwa ameishi maisha yake
yote akila chakula ambacho huliwa na watu wasiokula nyuma katika maisha yao. “Chakula
changu kikuu ni ugali na maharage.”
Rais Kikwete ateta na Watanzania
waishio Zambia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete usiku Jumatano, Februari 25, 2015, amekutana na kuzungumza na mamia
ya Watanzania waishio nchini Zambia, ikiwa sehemu ya ziara yake rasmi ya siku mbili
ya Kiserikali katika nchi hiyo. Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete alikutana
na Watanzania hao usiku kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia, ambako alipata nafasi
ya kujibu maswali yao na kuelezea kwa undani mafanikio ya maendeleo ambayo yanaendelea
kupatikana nchini.
Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza wa nje kualikwa
kutembelea rasmi Zambia tokea Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu
kushika madaraka ya dola mwezi uliopita, hatua inayoonyesha hali ya uhusiano mzuri
katika ya nchi hizo mbili jirani na marafiki.
“Ukisoma magazeti yetu nchini
na kufuatilia mijadala kwenye mitandao ya kijamii utadhani kuwa hakuna kinachofanyika
na kuwa nchi nzima inaongelea katika siasa tu. Lakini tunaendelea kufanya mambo mengi
iwe katika elimu, katika afya, kukabiliana na malaria na magonjwa wengine makubwa,
kupambana na ukimwi, kusambaza umeme vijijini, mapambano dhidi ya ujambazi na majambazi,
shughuli za miundombinu na ujenzi wa barabara pote tunafanya vizuri sana,”alisema
Rais Kikwete na kuongeza:
“Wakati Serikali yangu inaingia madaraka ni asilimia
10 tu ya vijiji vyetu vilikuwa na umeme, sasa tunazungumzia asilimia 45 ya vijiji
vya Tanzania vina umeme. Hapa tunazungumzia kiasi cha vijiji 5,000 kati ya vijiji
12,000 vya nchi yetu. Kwa ujumla, asilimia ya usambazaji umeme katika nchi yetu imepanda
kutoka asilimia 10 ya mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 36 kwa sasa. Siyo mafanikio
madogo hata kidogo.”
Kuhusu hali ya ujambazi nchini, Rais Kikwete amesema kuwa
upo ujambazi katika Tanzania, kama ilivyo kwa nchi zote duniani. “Lakini, hawa tutapambana
nao hawawezi kutushinda nguvu, tutazama nao na tutaibuka nao tu.” Rais Kikwete pia
ameelezea upanuzi mkubwa wa sekta ya elimu ikiwa ni elimu ya awali, ya sekondari na
ya juu. “Katika elimu ya juu, kwa mfano, wakati tunaingia madarakani idadi ya wanafunzi
katika vyuo vikuu vyote ilikuwa ni 40,000 tu lakini sasa tunazungumzia wanafunzi 200,000.”
Katika
afya, Rais Kikwete ameelezea uboreshaji mkubwa wa hospitali za mikoa na ujenzi wa
huduma nyingine za afya zikiwemo zahanati na vituo vya afya katika vijiji na kata
nchini. Aidha, Rais Kikwete amezungumzia hatua za kuongeza idadi ya madaktari nchini
akisema kuwa kwa sasa idadi ya madaktari wapya kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili
wameongezeka kutoka 200 hadi 400 kwa mwaka na kuwa idadi hiyo itakuwa kubwa zaidi
wakati ujenzi wa Hospitali ya Mlongazila, nje tu ya Dar es Salaam, utakapokamilika.
Rais
Kikwete pia alijibu maswali manane ya Watanzania hao ikiwa ni pamoja na lile kuhusu
uraia pacha, misamaha ya kodi kwa Watanzania wanaorejea nyumbani, mikopo kwa wanafunzi
wa kike wa Kitanzania ambao wanasomea masomo ya sayansi nje ya nchi, uwezekano wa
Benki ya CRDB kufungua tawi katika Zambia, hatua za Serikali kupunguza idadi ya vizuizi
vya barabarani, uwezekano wa Watanzania waishio nje kupata nafasi ya kupiga kura katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na jinsi gani Serikali ya Tanzania inaweza kuwasaidia Watanzania
waishio Zambia kufanya shughuli zao kwa uhuru zaidi.