2015-02-27 15:36:28

Si rahisi kutoa mafungo kwa Mapadre!


Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake wa karibu, Ijumaa asubuhi tarehe 27 Februari 2015 wamehitimisha mafungo ya maisha ya kiroho baada ya kukaa "Jangwani" kwa muda wa siku saba, huku wakisali na kufunga, wakitafakari na kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Mafungo haya yameongozwa na Padre Bruno Secondin, Jaalim mstaafu wa tasaufi mamboleo kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma. Mafungo haya yameongozwa na maneno ya Nabii Eliya.

Baba Mtakatifu kwa niaba ya wanamafungo wenzake, amemshukuru na kumpongeza Padre Bruno Secondin, Mkarmeli kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya maisha yao kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si rahisi kutoa mafungo ya maisha ya kiroho kwa Mapadre, kwani viongozi hawa wakati mwingine ni "watata", lakini Padre Secondin amefanikiwa kupandikiza mbegu ya Neno la Mungu.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Mwenyezi Mungu atawasaidia ili mbegu hii iweze kukua na kuzaa matunda yanayokusudiwa, huku wakitoka katika mafungo haya kwa kujivika Joho la Nabii Eliya, mikononi mwao, lakini zaidi mioyoni mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.