2015-02-27 12:28:43

Kutana na Chifu Mwakabulufu!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali imeamua kufufua bandari ndogo 14 kwenye mikoa mitatu inayozunguka Ziwa Nyasa ili kuimarisha
usafiri wa majini kwa wakazi wa Ruvuma, Njombe na Mbeya. “Tangu mwaka 2006 bandari za kwenye mikoa ya Ruvuma, Njombe na Mbeya zilikufa na hivyo kuleta shida ya usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo lakini Serikali imeamua kuzifufua bandari hizo na Itungi itakuwa ndiyo kituo kikuu cha bandari zote katika Ziwa Nyasa,” alisema Waziri Mkuu.


Alikuwa akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Kyela kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Jumatano, Februari 26, 2015 kwenye uwanja wa michezo wa Mwakangale na kuhudhuriwa na maelfu ya wakazi wa wilaya hiyo. Alizitaja bandari hizo kuwa ni Ndumbi, Lundu, Njambe, Mkili, Liuli, na Mbamba bay ambazo ziko mkoani Ruvuma. Nyingine ni Lumbila, Ifungu, Nsisi, Lupingu na Manda ambazo ziko Njombe wakati bandari za Mbeya ni Itungi, Kiwira na Matema.


Alisema ili kufanikisha hilo, Serikali imehamisha chelezo (Dry Dock) kutoka bandari ya Mwanza na kwamba mkandarasi kutoka Kampuni yaSongoro Marines, ameshaanza ujenzi wa chelezo hiyo. “Baada ya kukamilika, Chelezo hiyo, itatumika kutengenezea meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo na kufanya ukarabati wa meli pindi zinapohitaji matengenezo. Nimeambiwa na mkandarasi kutaka watamaliza hii kazi ifikapo Juni, mwaka huu,” alisema huku akishangiliwa na umati huo.


Waziri Mkuu alisema, mbali ya hilo, chelezo hiyo pia itatumikakutengeneza matishari mawili ya kubebea mizigo ambayo yatakuwa na uwezo wa kubeba mizigo tani 1,000 kila moja. “Yatatumika kusafirisha mizigo hiyo hususan mazao ya wakulima kupitia bandari ndogo zilizopo lakini pia yatasafirisha tani 60,000 za makaa ya mawe, tani 72,000 za saruji kutoka Mbeya kwenda Malawi na mikoa jirani; tani 10,000 za mbolea kutoka Dar es Salaam pamoja na chuma kutoka Liganga na Mchuchuma,” alisema.


“Chelezo hiki kitakapokamilika kitakuwa kikubwa na cha aina yake… hakuna kingine cha kulinganishwa nacho katika nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji. Itumieni fursa hii kwa kutunza ule mto kwenye mdomo wa kuingilia bandari ya Itungi, msilime kwenye kingo za mto,” aliongeza.

Mapema, akizungumza na wakazi wa kata ya Lusungo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Lusungo, Waziri Mkuu Pinda alisema daraja hilo ni kiungo muhimu kwenye barabara hiyo iendayo kwenye bandari ya Matema. Aliwataka wakazi wa kata hiyo walitunze daraja hilo ili liweze kuwasaidia kusafirisha bidhaa na mazao wanayolima. Ujenzi wa daraja hilo, ambalo limejengwa kupitia mfuko wa barabara, lina urefu wa mita 50 na upana wa mita 7.3 pamoja barabara yenye urefu wa mita 600 kutoka kwenye maingilio ya daraja hilo, limegharimu kiasi cha sh. bilioni 3.7 huku ujenzi wake ukiwa umekamilika kwa asilimia 99%.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda alipewa jina la MWAKABULUFU na Chifu Ernest Mwailemale wakati akisimikwa kuwa kiongozi wa eneo hilo la Lusungo. Waziri Mkuu alivishwa mgolole na kupewa mkuki ili autumie kuilinda nchi dhidi ya maadui kutoka pande zote. Akizungumza mara baada ya kumsimika Waziri Mkuu, Chifu Mwailemale mwenye umri wa miaka 91, alisema jina hilo ni la babu yake mzaa baba ambaye aliwahi kutawala eneo hilo. Hata hivyo, hakutaja ni mwaka gani.


Alipoulizwa maana ya jina hilo, Chifu Mwailemale ambaye wakati wote alikuwa akizungumza Kiswahili kwa ufasaha alisema: “Jina hili halina maana maalum bali na heshima kwa sababu lilikuwa la Chifu aliyetawala eneo hili,” alisema na kufafanua kuhusu umri wake: “Nina miaka 91 kwa maana nilizaliwa tarehe 25 Septemba mwaka 1924,” alisema Chifu huyo ambaye anaelezwa kupigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

MIMBA, UTORO KYELA VYAMTISHA WAZIRI MKUU

* 94 wapewa ujauzito, 645 watoroka shule wilayani humo

* Aaagiza waliohusika wasakwe, wafikishwe mahakamani


Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kyela pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuwasaka na kuwakamata wale wote waliowapa ujauzito wanafunzi na kuwafikisha mahakamani mara moja ili liwe fundisho kwa wengine. Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye shule ya sekondari ya Mwaya, kwenye kata za Ikusya na Lusungo na wakazi wa mji wa Kyela, Jumatano, Februari 26, 2015), Waziri Mkuu alisema elimu ni jambo la msingi sana kwa kizazi cha sasa na kijacho na Serikali haiwezi kuona fursa za elimu zikichezewa kiasi hicho. “Haiwezekani hata kidogo! Serikali hatuwezi kuwa tunahimiza ujenzi wa madarasa kila kukicha halafu watoto wanaopaswa kusoma kwenye hizo shule wao wanatoroka. Hawa watoto wana wazazi, iweje kuwe na utoro kiasi hiki?” alihoji.


“DED na DC wabaneni wazazi na mabinti walioharibiwa masomo, ni lazima watawataja wanaume waliohusika kuwapa mimba. Kwa kuanzia anzeni na hao wa mwaka jana ambao ni wasichana 11. Wakiwekwa ndani wachahe itakuwa fundisho kwa wengine,” alisema. Akielezea ukubwa wa wa tatizo hilo kwenye shule za sekondari peke yake, Waziri Mkuu alisema mwaka 2010, wasichana 26 walipewa ujauzito; mwaka 2011 (wasichana 22); mwaka 2012 (wasichana 19); mwaka 2013 (wasichana 16) na mwaka 2014 (wasichana 11). “Jumla yao ni 94, hii ni idadi kubwa sana. Akina baba waacheni watoto hawa wamalize masomo,
msiwaharibie maisha,” alikemea.


Akichanganua takwimu za utoro kwa wanafunzi haohao wa sekondari, Waziri Mkuu alisema mwaka 2010 walitoroka wanafunzi 95; mwaka 2011 (wanafunzi 160); mwaka 2012 (wanafunzi 212); mwaka 2013 (wanafunzi 90) na mwaka 2014 (wanafunzi 88). “Katika kipindi cha miaka mitano, jumla yao wote hawa ni 645. Hali hii haivumiliki na jambo liko ndani ya uwezo wa Halmashauri yenu. Fuatilieni wazazi wa hawa watoto na DC na DED ni lazima tabia hii ikomeshwe mara moja,” alionya.



Aliwaasa watoto wa wilaya wawe makini na masomo na waache tabia ya utoro na kupenda mambo ya maisha. “Wanangu someni kwa bidii, achaneni na haya mambo mengine. Ukipoteza nafasi masomo kidato cha tatu au cha nne, maisha yako yanakuwa yameharibika,” aliwaasa. Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwageukia wanaume wanaowafuata watoto wa shule na kuwataka kimapenzi wakati wanawake wa wilaya ni wengi kuliko wanaume. “Wlaya hii ina wanaume 106,012 na wanawake 115,478. Sasa ni kwa nini msiwafuate hao akinamama wakubwa ambao ni wengi kuliko ninyi? Acheni huo mchezo, waacheni hawa watoto wa kike wamalize masomo yao,” alisisitiza.

Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Bi. Margareth Malenga alisema kushamiri kwa biashara kwenye mpaka wa Kasumulu, mkoani Mbeya, kumechochea kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaotoroka shuleni na kwenda kujishughulisha na biashara ndogondogo mpakani hapo.


“Aidha, kukosekana kwa chakula kwenye baadhi ya shule za msingi na sekondari wilayani hamu, ni sababu nyingine inayofanya wanafunzi waache masomo na kwenda kufanya biashara ndogondogo kwenye mpaka wa Kasumulu,” aliongeza. Alisema hali hiyo imechangiwa na kuwepo kwa baadhi ya kaya masikini zinazoshindwa kuwalipia gharama za masomo watoto wao. Akifafanua, Bi. Malenga alisema katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2014, wavulana 414 na wasichana 159 waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari waliacha shule kwa sababu za utoro.


Kuhusu elimu ya msingi, Bi. Malenga alisema, wanafunzi wapatao 711 wametoroka shule lakini kutokana na jitihada zilizofanyika, wanafunzi 155 wamerudishwa shuleni. “Wanafunzi 556 waliobakia wanaendelea kutafutwa kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji ili waweze kuwarudishwa kuendelea na masomo,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wameanzisha utaratibu wa kila Mkuu wa Shule kuwasilisha ripoti ya mahudhurio ya wanafunzi kwa watendaji wa kata na vijiji kila Ijumaa ambapo tangu utaratibu huo uanze, wamefanikiwa kudhibiti utoro kwa asilimia 91%.








All the contents on this site are copyrighted ©.