Magereza panapaswa kuwa ni mahali ambapo mkosaji anapata fursa ya kuweza kujirekebisha
kutokana na mapungufu yake, ili anapohitimisha adhabu yake, aweze kurudi tena ndani
ya jamii na kuendelea vyema na maisha. Kwa miaka mingi mageregza nchini Malawi yalikuwa
yanatisha kwa kutozingatia haki msingi za binadamu, utu na heshima yao, lakini hali
kwa sasa imeanza kubadilika na kuboresha kutokana na changamoto kubwa iliyotolewa
na Rais Arthur Peter Mutharika wa Malawi wakati alipokuwa anafunga mafunzo ya Askari
Magereza 731 hivi karibuni.
Katika hotuba yake, Rais Mutharika aliwaambia
Askari Magereza wamepewa dhamana ya kusaidia kurekebisha mwenendo wa wafungwa ili
waweze kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi na wala si kwa ajili ya kuwashikisha
adabu. wachunguzi wa mambo wanasema, mambo yanabadilika pengine ni kutokana na ukweli
kwamba, hata Rais mwenyewe alikwishawahi kuonja suluba ya kukaa Lupango", akashuhudia
jinsi ambavyo magereza yalivyokuwa yamefurika kiasi cha kutishia usalama na maisha
ya wafungwa na Askari Magereza wenyewe.
Sheria na marekebisho ya magereza ni
mambo ambayo yanapokelewa kwa mikono miwili na wananchi wengi wa Malawi, hii ikiwa
ni pamoja na kuwasaidia wafungwa kutumikia vifungo vyao nje ya magereza kwa kufanya
shughuli mbali mbali za kijamii badala ya kukaa muda wote magerezani. Hapa wachunguzi
wa mambo wanasema, Serikali pia haina budi kuangalia mishahara na mazingira ambamo
Askari Magereza wanafanyia kazi, ili kufanya maboresho makubwa zaidi katika kulinda
na kudumisha utu na heshima ya binadamu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.