2015-02-26 09:33:55

Msiwagawe watu kwa udini na ukabila!


Askofu mkuu Martin Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, hivi karibuni amesimikwa rasmi na kukabidhiwa jukumu la kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu Jimbo kuu la Mombasa, baada ya kuteuliwa hivi na Baba Mtakatifu Francisko kutoka Jimbo Katoliki la Machakosi. Ibada hii ya Misa takatifu imeongozwa na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka nchini Kenya.
Kardinali Njue amewaambia waamini kwamba, huu ulikuwa ni mwanzo wa ukurasa mpya wa historia ya Jimbo kuu la Mombasa, ambao wanapaswa kuchangia kuuandika kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, ili Kanisa liweze kung’ara na kushamiri. Amewataka Wakleri, Watawa na Waamini katika ujumla wao, kuonesha mshikamano wa dhati na Askofu mkuu Kivuva ili aweze kutekeleza majukumu yake barabara, tayari kuionjesha Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa, Furaha ya Injili kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Kardinali Njue ameitaka Familia ya Mungu nchini Kenya kuhakikisha kwamba, inajenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa kama sehemu ya utambulisho wao na kamwe wasikubali kugawanywa kwa misingi ya ukabila wala udini. Amewataka wanasiasa kuchuchumilia umoja na mshikamano wa kitaifa kama sehemu ya mchakato wa kuwaletea wananchi maendeleo endelevu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao na ustawi wa wananchi wote wa Kenya.

Kardinali Njue anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Kenya kusimama kidete ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu kwa kukumbatia Injili ya Uhai ili kukataaa sera na mikakati inayotaka kuwatumbukiza katika utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha uzazi salama. Wananchi wa Kenya waendelee kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuimarisha amani na maridhiano kati ya watu.
Askofu mkuu Kivuva amemshukuru kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwamini na kumdhaminisha kuongoza Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Mombasa. Anaendelea kujiweka chini ya ulinzi wa Yesu Kristo mchungaji mkuu katika utekelezaji wa majukumu yake kadiri ya mpango wa Mungu. Amewashukuru waamini kutoka Jimbo Katoliki la Machakosi kwa ushirikiano ulioliwezesha Kanisa kukua na kupanuka kutoka Parokia 41 alizokabidhiwa wakati alipoteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Machakosi, hadi kufikia Parokia 78, kweli haya ni matendo makuu ya Mungu yanayojionesha kwa njia ya umoja, ushirikiano na mshikamano kama Familia ya Mungu inayotembea pamoja.
Askofu mkuu Kivuva anasema, mipango yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jimbo kuu la Mombasa ni kadiri ya maelekezo ya Kristo mwenyewe, yaani kuhakikisha kwamba, anaendelea kujisadaka kwa ajili ya wokovu wa wengi na kwamba, anapenda wote waweze kuokolewa na kupata utimilifu wa maisha. Ni mkakati wake wa kichungaji kwamba, wote wawe wamoja, chini ya mchungaji mkuu, yaani Yesu Kristo!
Naye Askofu mkuu Charles Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Sudan ya Kusini, katika Ibada ya Misa Takatifu kumuaga Askofu mkuu Martin Kivuva kutoka Jimbo Katoliki la Machakos, amewataka waamini kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia tena mchungaji mwingine atakaendeleza kazi za kichungaji zilizoachwa na Askofu mkuu Kivuva. Kuteuliwa kuwa Askofu mkuu ni wajibu mzito na wenye dhamana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa.

Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA na wadau wengine!








All the contents on this site are copyrighted ©.