2015-02-26 09:15:41

Jubilee ya miaka 50 tangu Ibada ya Misa ilipoadhimishwa kwa mara ya kwanza kwa Lugha ya Kiitalia!


Mwenyeheri Paulo VI kunako tarehe 7 Machi 1965, miaka 50 iliyopita aliadhimisha kwa mara ya kwanza Ibada ya Misa Takatifu kwa lugha ya Kiitalia katika Parokia ya Watakatifu Wote, iliyoko Jimbo kuu la Roma kama sehemu ya utekelezaji wa mageuzi yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kutambua kwamba, Liturujia ni kilele na chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa.

Marekebisho ya sheria na kanuni za Liturujia yalipaswa kuzingatia hali za watu na mapokeo yao. Itakumbukwa kwamba, kwa miaka mingi Kanisa liliadhimisha Mafumbo matakatifu kwa njia ya Lugha ya Kilatini, lakini tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, waamini katika nchi mbali mbali wanaweza kumwabudu, kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa lugha zao mahalia, matendo makuu ya Mungu.

Mwenyeheri Paulo VI katika mahubiri yake aliwakumbusha waamini kwamba, huu ulikuwa ni mwanzo wa matumizi ya lugha mbali mbali katika Liturujia ya Kanisa, ili kumwezesha mwanadamu kujadiliana na Mwenyezi Mungu kwa kutumia lugha anayoifahamu. Jimbo kuu la Roma, hapo tarehe 7 Machi 2015, Baba Mtakatifu ataadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Ibada ya Misa Takatifu ilipoadhimishwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya Kiitalia, kwenye Parokia ya Watakatifu wote, Jimbo kuu la Roma.

Tukio hili la kihistoria linakumbukwa kwa njia ya makongamano na semina, ili kuwaelimisha waamini lengo na madhumuni ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika mageuzi ya maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliwataka waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na kamwe wasiwe ni watazamaji!.







All the contents on this site are copyrighted ©.