2015-02-25 10:08:26

Waendeeni wale walioko pembezoni mwa Jamii!


Kardinali Manuel Josè Macàrio do Nascimento, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kutoka huko lilikojifungia kwa miaka nenda miaka rudi, tayari kuwaendelea maskini wa maisha ya kiroho na kimwili pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha Injili ya Furaha na Matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Kardinali Do Nascimento ni kati ya Makardinali wapya waliotangazwa na kusimikwa na Baba Mtakatiffu Francisko hivi karibuni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema, amepokea dhamana na utume huu kwa moyo mnyofu na ari kuu kwa kutambua kwamba, Baba Mtakatifu anawachangamotisha kujikita katika mshikamano wa kidugu, huruma na upendo wa Mungu, mambo makuu yanayojitokeza zaidi na zaidi katika Waraka wake wake kichungaji, Injili ya Furaha, "Evangelii gaudium".

Kardinali Do Nascimento anasema, leo hii kuna umati mkubwa wa watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha. Ni watu wanaotengwa na jamii na kujikuta wakielemewa katika upweke hasi, ambao mara nyingi ni chanzo cha watu kukata tamaa na hivyo kupoteza ladha na utamu wa maisha. Utandawazi unaendelea kuwagawa watu badala ya kuwaimarisha, kwani leo hii ulimwengu ni kama kijiji, lakini watu hawafahamiani, wanaogopana na kutishana.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni kati ya mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa umaskini wa hali na kipato miongoni mwa wananchi wengi wa Bara la Ulaya na pengine duniani kote. Watu wengi hawana fursa za ajira kutokana na uzalishaji na uwezo mdogo wa wananchi kununua bidhaa na huduma inayotolewa sokoni. Watu wamekata tamaa, kumbe ni jukumu la Mama Kanisa kusaidia mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Matumaini inayojikita katika mshikamano wa udugu na upendo kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linaendelea kuwafunda watu mbinu na mikakati ya kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kwa kujikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa mambo makuu manne yaani: utu na heshima ya binadamu; mafao ya wengi; kanuni auni na mshikamano wa kidugu. Barani Ulaya kama ilivyo pia nchini Hispania kuna sera mbali mbali za kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, lakini Kanisa linapenda kujikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Kutokana na watu wengi kuanza kumezwa mno na utamaduni wa kifo kwa kushindwa kutambua na kuthamini zawadi ya maisha, kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wanaotema zawadi ya maisha kwa kujinyonga, kwani wanashindwa kutekeleza sera na mikakati ya uchumi ambayo haigusi mateso na mahangaiko ya watu wa kawaida; huu ni uchumi usiojali na matokeo yake ni vifo kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Kardinali Do Nacimento anasema, Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wengi nchini Ureno ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wake; katika unyenyekevu na unyofu wa moyo; katika huruma na mapendo yanayojikita katika mshikamano wa kidugu, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu hata katika tofauti zao, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini. Hii ndiyo changamoto inayofanyiwa kazi na Jimbo kuu la Lisbon, Ureno katika mikakati na shughuli za kichungaji.

Kunako mwaka 2016, Jimbo kuu la Lisbon litaadhimisha Sinodi ya Jimbo kwa kuishirikisha Familia ya Mungu Jimboni humo, ili kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Injili ya Furaha, Evangelii gaudium. Waraka huu ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa, mwaliko wa kuzivalia njuga changamoto hizi ili kuzifanyia kazi katika hali ya unyofu, ili kweli Familia ya Mungu iweze kuonja huruma na mapendo ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.