Amani, utulivu, maendeleo na maridhiano ndani ya Jamii yanategemea kwa kiasi kikubwa
ubora wa maisha ya ndoa na familia. Hiki ndicho kiini cha ujumbe wa Askofu Maurice
Piat wa Jimbo Katoliki la Port-Louis, nchini Mauritius katika barua yake ya kichungaji
kwa ajili ya Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima inayoongozwa na kauli mbiu "Jamani
familia, Mungu anawapenda".
Licha ya mambo kadhaa yanayohatarisha mshikamano
na mfungamano wa maisha ya ndoa na familia, bado Wakristo na watu wote wenye mapenzi
mema hawana budi kujifunga kibwebwe ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza
Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko; maisha yanayojikita
katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia!
Wanafamilia watambue changamoto
zilizoko mbele yao ili kweli waweze kuzikabili kwa imani, matumaini na mapendo, kwa
kumegeana na kuonjesha uzuri wa maisha ya kuishi na kushibana kwa pamoja kama wanandoa.
Pale wanandoa wanapokosa muda na nafasi ya kuonana, kusaidiana na kufarijiana, hapo
kasoro na cheche za majanga ya maisha ya ndoa na familia zinaanza kuojionesha. Wanandoa
wawe na ujasiri wa kushirikishana magumu na matumaini ya maisha, katika ukweli na
uwazi, ili kuponya madonda na majeraha yanayoweza kuwa yamejitokeza katika hija ya
maisha yao.
Askofu Maurice Piat anasema kinzani kati ya Baba na Mama ndani
ya familia na hatimaye kutalakiana, ni mambo ambayo yanaacha kurasa chungu katika
maisha, malezi na makuzi ya watoto. Pale baba wa familia anapoamua kuchukua "kidumu"
au kung'ang'ania kwenye "nyumba dogo" hapo majanga yanaanza kuingia katika maisha
ya kifamilia na kwamba, mwelekeo kama huu unaweza kumfanya mama pia kutaka kumkomoa
mwenzi wake wa ndoa kwa "kwenda chocho", mambo ambayo yanahatarisha, amani, ustawi
na maendeleo ya maisha ya ndoa na familia.
Inasikitisha kuona kwamba, kuna
idadi kubwa ya familia tenge, zinazosimamiwa na kuendeshwa na mzazi mmoja na mara
nyingi ni mwanamke ambaye anajikuta akilazimika kuwahudumia watoto wake, hata kama
ni kwa shida kubwa. Ni wanawake wanaojitaabisha kuwaelimisha watoto wao na kuhakikisha
kwamba, wanapata maisha mazuri kama watoto wengine, lakini wakati mwingine, wanashindwa
na kuelemewa na mzigo wa malezi na makuzi ya watoto; matokeo yake watoto wanajisikia
kutokuwa na ulinzi na usalama, hivyo wanaweza kujikuta wanaishi katika mazingira magumu
na hatarishi.
Askofu Maurice Piat anasema kwamba, kuna mambo ambayo yanafumbatwa
katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; mambo ambayo
yanaathari kubwa kwa maisha na utume wa ndoa na familia, ikiwa kama hayataweza kuangaliwa
kwa umakini mkubwa. Si familia zote zinazoweza kuridhisha matakwa na matamanio ya
watoto wao; jambo hili lisipoeleweka, kuna hatari ya amani na mfungamano wa maisha
ya kifamilia kutoweka.
Wazazi wajitahidi kujenga utamaduni wa kuwa karibu
zaidi na watoto wao hasa wakati huu wa kipindi cha mpito kuelekea utandawazi usiojali
wala kuguswa na masuala ya imani, maadili na utu wema. Wanandoa wajifunze kujikita
katika ukweli na uwazi kwa njia ya majadiliano, ili kutambua hali halisi ya maisha.
Askofu
Maurice Piat katika ujumbe wake wa Kwaresima anasema kwamba, Mapadre, Watawa na Waamini
walei wanayodhamana ya kulinda, kutetea na kudumisha misingi bora ya maisha ya ndoa
na familia, ndiyo maana Kanisa halina budi kuwa karibu na familia zinazoogelea katika
shida na mahangaiko makubwa, kwa kuzionjesha upendo, mshikamano na matumaini. Utume
huu unaweza kutekelezwa vyema zaidi kwa njia ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo.
Waamini
wafahamishwe maana na umuhimu wa mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia,
ili wawezwe kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao, tayari kuwatangazia Watu wa
Mataifa, Injili ya Familia, vinginevyo watu wanaweza kuwa na ufahamu hasi kuhusu Kanisa,
kiasi cha kuwaachia madonda ya kudumu katika hija ya maisha yao ya kila siku.
Kanisa
halina budi kuhakikisha kwamba, linawatangazia Watu wa Mataifa, Habari Njema ya Wokovu,
tayari kutoka ili kuwaendea wale wote wenye kiu na njaa ya kutaka kusikiliza Injili
ya Kristo, tayari kukumbatia wokovu unaoletwa na Yesu Kristo. Hawa ni watu wanaopaswa
kusikilizwa na kusaidiwa katika ukweli na uwazi; katika imani, mapendo na matumaini,
ili waweze kukutana na Yesu Kristo mchungaji mwema, mwingi wa huruma na mapendo; aliyekuja
si kwa ajili ya kuwahukumu watu, bali kutoa maisha yake, ili yaweze kuwa ni fidia
ya wengi.
Askofu Maurice Piat katika barua yake ya kichungaji wakati huu wa
Kwaresima, anawaalika viongozi wa Serikali kutoa kipaumbele kinachostahili katika
sera na mikakati yao ya maendeleo, kwa kutambua kwamba, familia ni rasilimali muhimu
sana katika mchakato wa kukoleza na kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii. Wananchi
waelimishwe umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha, maadili
na utu wema; wafundwe umuhimu wa kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi;
waoneshe upendo na ukarimu kwa jirani, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
jamii na kwamba, familia ni shule ya utakatifu, haki, amani na maridhiano ndani ya
jamii.
Askofu Maurice Piat anahitimisha ujumbe wake wa Kwaresima kwa kukumbusha
kwamba, amani, utulivu na haki jamii ni mambo yanayotegemea kwa kiasi kikubwa ubora
wa maisha ya kifamilia. Ni wajibu wa Serikali na wadau mbali mbali kuweka mikakari
na sera makini kwa ajili ya kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Mama
Kanisa kwa upande wake, ataendelea kuchangia katika mchakato wa ustawi na maendeleo
familia kwa kushirikiana na kujadiliana na wadau mbali mbali, ili kweli familia iweze
kutekeleza dhamana na wajibu wake ndani ya jamii.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.