2015-02-25 14:20:36

Juhudi za kukomesha biashara haramu ya madini Afrika


Ukomeshaji wa unyonyaji watoto, wanaume na wanawake unaofanywa katika biashara haramu ya madini, ni lengo kuu la kampeni iliyoanzishwa na Focsiv, ambalo ni Shirikisho la Mashirika ya Kimataifa ya huduma za kujitolea “Voluntary Service” na kwa ushirikiano wa Maaskofu 125 , kama alivyoeleza mratibu wa "sera" wa Focsiv, Bwana Andrea Stocchiero.

Amesema kwa bahati mbaya kwa miaka mingi, madini yameendelea kuporwa na mabapari, na kushamirisha biashara hii kwa kutumia wakazi wa mitaani , ikiwa ni pamoja na watoto kulazimishwa kufanya kazi katika migodi na makundi ya “wababe", wenye silaha, ambao wanasababisha uwepo wa mikopo makubwa kutokana na biashara hii haramu ya madini, yenye kusaidia pia uwepo wa manunuzi hata ya silaha za moto na hatari, zenye kuzua migogoro mipya na vurugu miongoni mwa watu.

Stocchiero, ameyataja maeneo yaliyoathirika zaidi na biashara haramu ya madini barani Afrika kuwa ni Afrika ya Kati hasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na nchi jirani. Pamoja na kwamba Marekani miaka minne iliyopita iliweka sheria inayodai makampuni kuhakikisha hawanunui madini kutoka vyanzo haramu, sheria hiyo imekuwa haina nguvu. Maeneo mengine pia ni barani Asia, hasa katika maeneo ya mipakani na pia Amerika ya Kusini ambapo maeneo kama vile Colombia, Venezuela na Peru , kumekuwa na sifa za uwepo wa mashirika ya jinai, yanayoshamirishwa na biashara haramu ya madini.

Aidha ameeleza ombi la taasisi yake ya Focsiv kwa Umoja wa Ulaya kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kupitisha kanuni thabiti inayodai makampuni yanayofanya biashara ya madini, kuthibitisha kwamba biashara yao wanaifanya kwa mujibu wa sheria, pia kuhamasisha makampuni ya kuwa sehemu ya uwazi katika daftari la ya biashara, lenye kuonyesha uhalali wa idhaa zake. Ombi la pili ni kuhakikisha kwamba kanuni hii ni pamoja na madini ya chuma, bati na Tungsten na shaba n.k ambayo kwa miaka mingi hayakutiliwa maanani kama ni kati ya biashara haramu yenye kuzua migogoro. Na tatu ni makampuni ya biashara ya madini kuona kuwa ni wajibu wa kuthibitisha mali ghafi zimetoka wapi.

Kwa maono hayo, FOCSIV, kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali, wanajaribu kuongeza ufahamu miongoni mwa wanasiasa na hasa wabunge kupigia kura ya ndiyo sheria hiyo. Na pia kushirikiana na Maaskofu katika hatua za pamoja na majimbo, kwa ajili ya kukusanya taarifa mbalimbali katika maeneo yao juu ya matukio mbalimbali.

FOCSIV, inaona umuhimu wa kuongeza uelewa wa maoni ya umma juu ya suala hili, ili kwamba biashara hii ya madini iwe kwa manufaa ya jamii yote na si tu kwa manufaa ya kundi dogo la wanyonyaji. Inaita biashara zote zinazofanyika kinyume cha sheria kuwa ni kashfa kubwa kwa binadamu. Kwa wananchi kuwa na ufahamu wa kutosha wanaweza kukabiliana na makampuni yanayofanya biashara ya madini kimagendo.








All the contents on this site are copyrighted ©.