2015-02-25 11:02:16

Hongera Askofu mteule Sangu!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Pongezi Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (T.E.C) na Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, kufuatia uteuzi uliofanywa na Baba Mtakatifu Francisko, wa Monsinyo Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki Sumbawanga kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.

Askofu Mteule Liberatus Sangu aliyekuwa Afisa mwandamizi katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu mjini Vatican, anatarajiwa kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo la Shinyanga tarehe 12 Aprili, 2015. “Nachukua fursa hii kukupongeza kwa dhati kabisa kwa mafanikio ambayo Kanisa Katoliki hapa nchini limeendelea kuyapata, kufuatia kuteuliwa kwa Monsinyo Liberatus Sangu kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki la Shinyanga.

“Hii inadhihirisha wazi kutambuliwa kwa mchango mkubwa wa Padre Sangu katika kuwatumikia kikamilifu Kondoo wa Bwana hususan kupitia Idara nyeti ya Uenezaji wa Injili kwa Mataifa aliyokuwa akiitumikia akiwa mjini Vatican ambako ndiyo Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani”, amesema Rais Kikwete katika pongezi zake.

Rais Kikwete amemuomba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kumfikishia Salamu zake za Pongezi kwa Askofu Mteule Liberatus Sangu kwa kuteuliwa kwake, na amemtakia mafanikio zaidi katika Wadhifa wake Mpya wa Askofu katika kulitumikia Kanisa Katoliki na Wamini wa Kanisa hilo kwa ujumla hapa nchini, hususan katika Jimbo Katoliki la Shinyanga alikopangiwa kwenda kufanya kazi.








All the contents on this site are copyrighted ©.