2015-02-25 10:42:18

Dumisheni majadiliano ya kidini!


Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni mashahidi wa Kristo na Kanisa lake, kwa kuendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya kanuni msingi za maisha ya Kiinjili, ili kuonesha umuhimu wa imani inayomwilishwa katika maisha na mikakati ya watu na wala si jambo la kuwekwa pembezoni mwa maisha!

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Benjamin Ndiaye, wakati wa Ibada ya kumsimika kuwa Askofu mkuu mpya baada ya Kardinali Theodore Adrein Sarr, kung'atuka kutoka madarakani hivi karibuni. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka Senegal. Askofu mkuu Ndiaye, amewataka waamini kuimarisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kuendelea kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini watambue mafundisho tanzu ya Kanisa kama yanavyofafanuliwa katika: Biblia, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Waamini wajenge na kuimarisha umoja na mshikamano hata katika tofauti zao za karama na vipaji; waimarishe ukarimu kwa wageni na maskini; mambo msingi ambayo, Maaskofu Katoliki Senegal, walikumbushwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yao ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dakar, ishikamane katika umoja na udugu; katika huduma na ibada, ili Mwenyezi Mungu aweze kupewa sifa na utukufu na mwanadamu kupata ustawi na maendeleo ya kiroho na kimwili.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Luis Mariano Montemoyor, Balozi wa Vatican nchini Senegal amewataka waamini kuendeleza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi na waamini wa dini ya Kiislam pamoja na taasisi mbali mbali nchini humo, ili kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kusimama kidete kwa ajili ya kutafuta na kudumisha mafao ya wengi.

Wakristo na Waislam nchini Senegal wanapaswa kuheshimiana na kushirikiana licha ya changamoto za utengano na kinzani zinazoendelea kuoneshwa sehemu mbali mbali za dunia.

Naye Kardinali Thèodore Adrian Sarr, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, ameishukuru Familia ya Mungu nchini Senegal kwa ushirikiano waliomwonesha wakati alipokuwa kiongozi mkuu wa Jimbo kuu la Dakar, anawataka sasa kuendelea kujielekeza katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano ndani ya jamii, kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.