Kardinali Andrè Vingt-Trois, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa katika ujumbe
wake wa Kwaresima kwa mwaka 2015 anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi
mema kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha jirani zao ile furaha inayobubujika kutoka
katika imani kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kuwamegea na kuwaonjesha maskini matendo
ya huruma na mapendo pamoja na kuwashirikisha vijana matumaini kwa leo na kesho iliyo
bora zaidi.
Kuwashirikisha wengine ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka
kwa Kristo na Kanisa lake kuna maanisha ya kuwatangazia Watu wa Mataifa kuhusu: Yesu
Kristo aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, ili kumkomboa
mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Hii ndiyo changamoto kubwa ambayo
Baba Mtakatifu Francisko anaibainisha katika Waraka wake wa kichungaji Furaha ya Injili,
"Evangelii gaudium".
Hapa waamini wanachangamotishwa kusimama kidete na kamwe
wasikubali wajanja wachache kuwapoka ari na nguvu ya kimissionari, bali wahakikishe
kwamba, kila wakati wanaendelea kujipyaisha, ili kuwafikia watu wengi zaidi, ili kuwaonjesha
Injili ya Furaha na Matumaini; kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mashiko na mvuto!
Kardinali
Andrè Vingt-Trous anasema vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa, kwani wanaweza kutangaza,
kushuhudia na kuwashirikisha wengine tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii.
Ndiyo maana kuna haja kwa familia na shule kushirikiana kwa dhati kabisa kwa ajili
ya ustawi na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya, kila upande ukitekeleza dhamana
na wajibu wake barabara.
Vijana warithishwe tunu msingi za maisha ya kiroho,
kiutu na kimaadili, zitakazowasaidia kuwajibika barabara kwa maneno na matendo yao.
Vijana wasigeuzwe kuwa ni madodoki ya kupokea kila takataka inayotolewa kwenye vyombo
vya habari na mitandao ya kijamii.
Vijana wajengewe utamaduni wa kujisadaka
na kutoa huduma kwa ajili ya jirani zao; wawe ni wajenzi badala ya kugeuzwa kuwa ni
walaji wa kupindukia. Kwa Wakristo, vijana washirikishwe tangu mwanzo cheche za imani,
matumaini na mapendo., kamwe wasikubali imani yao itekwe nyara na wajanja wachache
kwa ajili ya mafao yao binafsi.
Kardinali Vingt-Trois, Askofu mkuu wa Jimbo
kuu la Paris, Ufaransa anahitimisha ujumbe wake wa Kwaresima kwa kuyaelekeza macho
yake kwenye maadhimisho ya mkutano mkuu wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi
unaotarajiwa kufanyika nchini Ufaransa, Mwezi Desemba 2015. Kwa Familia ya Mungu nchini
Ufaransa, huu ni wakati muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu tabia na mtindo
wao wa maisha, ili kuhakikisha kwamba, wanakuwa na matumizi bora ya rasilimali za
dunia, hali ambayo haina budi kujikita katika mfumo wa maisha.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.