2015-02-24 10:13:05

Wanawake Colombia watunukiwa tuzo ya amani kwa mwaka 2015


Chama cha Kimataifa cha amani, Pax Christi, kwa mwaka 2015 kimeamua kuwatunukia tuzo la amani Mtandao wa wanawake kutoka nchini Colombia kwa kutambua mchango wao katika tafakari na matendo ambayo yameiwezesha Colombia kuanza tena mchakato wa amani na utulivu baada ya kuogelea kwa muda mrefu katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, iliyosababisha maafa makubwa kwa watu.

Pax Christi inapenda kuwahamasisha wanawake kuchangia katika ustawi, maendeleo, amani na utulivu katika familia, jamii na nchi zao, kwani hawa ni watu wenye uwezo mkubwa na wanaweza kufanikisha azma hii, ikiwa kama watawezeshwa kikamilifu. Wanawake wamekuwa ni walimu wazuri wa maadili na utu wema ndani ya jamii, mambo ambayo yameliwezesha taifa la Colombia kuanza mchakato wa msamaha na upatanisho kwa ajili ya mafao ya wengi. Watu wakijikita katika maadili, amani na utulivu vinaweza kupatikana.

Mtandao wa wanawake kutoka Colombia ulianzishwa Mwezi Oktoba 2011 ili kuwaunganisha wanawake kutoka katika medani mbali mbali za maisha na dini, ili kwa pamoja wasaidie kuifunda jamii kujikita katika maadili na utu wema, ili amani ya kweli iweze kupatikana nchini Colombia. Pax Christi linasema kwamba, hapa tofauti za kidini, kisiasa na kijamii umesaidia kuwaunganisha watu kwa ajili ya mafao ya wengi na leo hii amani imepatikana. Kanuni maadili ni nguzo msingi katika kukoleza mabadiliko ndani ya jamii.

Pax Christi inawapongeza wanawake kwa kujifunga kibwebwe haki kuhakikisha kwamba, amani na upatanisho vinashika kasi tena nchini Colombia. Yote haya yamewezekana kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maadili, utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Pax Christi inawapongeza wanawake kwa mchango wao makini katika kukuza na kudumisha amani na maridhiano ndani ya jamii.

Mtandao wa wanawake kutoka Colombia utakabidhiwa tuzo lao hapo tarehe 16 Mei 2015 huko mjini Bethlehemu wakati Pax Christi itakapokuwa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Tuzo ya amani ilianza kutolewa na Pax Christi kunako mwaka 1988 ili kutambua juhudi za watu mbali mbali katika kukuza na kudumisha amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.