2015-02-24 11:54:05

Tumetoka mbali, miaka 100 si haba!


Mfuateni Kristo katika uhalisia wa maisha yenu, ndiyo kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho ya Jubilee ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Bikira Maria, Kitgum, Jimbo kuu la Gulu, Uganda, iliyofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu nchini Uganda. Hizi ni juhudi za Wamissionari wa Comboni zilizoanzishwa kunako mwaka 1911, kwa kupandikiza mbegu ya Ukristo, leo hii matunda yanaonekana, lakini hayana budi kuimarishwa na kutolewa ushuhuda wa maisha.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Michael Augustin Blume, ameitaka Familia ya Mungu nchini Uganda kumkumbatia Kristo katika maisha na vipaumbele vyao, kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo, ili kuliwezesha Kanisa kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika medani mbali mbali za maisha. Changamoto hizi ni zile zinazojikita katika utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia bila kusahau ukanamungu.

Kanisa nchini Uganda halina budi kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, ili kusaidia mchakato wa kuwafunda vijana tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Kuna haja ya kuachana na mila pamoja na desturi zilizopitwa na wakati na zile ambazo kimsingi zinasigana na tunu msingi za Kiinjili, kiasi cha kuwapotosha watu.

Yesu Kristo ndiye Mkombozi wao, changamoto na mwaliko kwa vijana kukumbatia maisha ya Kisakramenti kwa kuthubutu kupokea Sakramenti ya Ndoa Takatifu, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia, kwa njia ya ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Vijana wahakikishe kwamba, wanajitafutia ajira ili kujipatia mahitaji yao msingi.

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Bikira Maria, Kitgum, Jimbo kuu la Gulu. Rais Museven amechangia millioni 30 za Uganda, ili zisaidie mchakato wa maendeleo kwa Familia ya Mungu Parokiani hapo. Ameliomba Kanisa nchini Uganda kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya baa la umaskini kwa kuwajengea waamini wake uwezo wa kujitegemea na kujiendeleza. Viongozi wa Kanisa wawe ni mfano bora katika mapambano dhidi ya umaskini. Sherehe hizi zimehudhuriwa na umati mkubwa kutoka ndani na nje ya Uganda, kwani kwa hakika miaka 100 si haba!







All the contents on this site are copyrighted ©.