2015-02-24 10:18:57

Silaha za mapambano wakati wa Kwaresima!


Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, Italia, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika kipindi hiki cha Kwaresima kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuiamini Injili pamoja na kuhakikisha kwamba, kila siku wanajitahidi kuboresha maisha na utu wao wa ndani kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Toba na wongofu wa ndani ni mwaliko wa kutubu dhambi sanjari na kurekebisha mapungufu ya kibinadamu, kwa njia ya ushuhuda makini kutoka kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Kwaresima ni kipindi kilichokubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu, mwaliko kwa waamini kuzama katika maisha ya sala, toba, kufunga, kutafakari pamoja na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha, kwani hii ndiyo chemchemi ya mapendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwaresima ni kipindi ambacho Mama Kanisa anawaalika Wakristo kupyaisha tena utambulisho wao wa Kikristo kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Mapambano kati ya Yesu na Shetani kule Jangwani kwa siku arobaini, iwe ni changamoto kwa Wakristo kutambua kwamba, wasipokuwa makini, Shetani anaweza kutumia baa la njaa kuwavuruga. Kwaresima, kiwe ni kipindi cha mshikamano na watu wanaoteseka kwa baa la njaa duniani.

Waamini wawe macho na kishawishi cha kupenda mno madaraka, kiasi hata cha kumezwa na malimwengu, bali daima wajitahidi kumwangalia Yesu Kristo aliyetundikwa pale Msalabani, chemchemi ya upendo, amani na uhuru wa kweli. Kristo ndiye anayepaswa kuheshimiwa, kuabudiwa na kutukuzwa kwani kwa njia ya Fumbo la Msalaba ameukomboa ulimwengu.

Mapambano ya maisha ya kiroho katika kipindi hiki cha Kwaresima yanajikita katika sala na kufunga ili kuratibu na kurekebisha vilema vinavyomwandama mwamini katika hija ya maisha yake hapa duniani. Waamini washinde kishawishi cha uvivu pale wanapoweza washiriki hata Ibada ya Misa Takatifu kati kati ya juma, bila kusahau umuhimu wa Njia ya Msalaba. Kwaresima ni kipindi cha kukikimbilia upendo na huruma ya Mungu katika maisha kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.