Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM limemteua
Bwana Berhanu Tamene Woldeyohannes, Mratibu wa Tume ya haki na amani ya SECAM kuwa
mwakilishi wa SECAM kwenye Umoja wa Afrika, wenye Makao yake makuu mjini Addis Ababa,
Ethiopia. Amekabidhiwa wajibu wa kuharakisha mchakato wa mahusiano kati ya Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM pamoja na Umoja wa Afrika.
Lengo ni kuliwezesha Kanisa kushiriki kikamilifu katika mchakato unaopania
kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Bara la Afrika; kwa kujikita katika uongozi
na utawala bora unaosimamia maendeleo endelevu ya Familia ya Mungu Barani Afrika.
SECAM inapenda kuchangia katika mchakato wa misingi ya usawa, haki, amani na upatanisho.
Bwana Woldeyohannes atakuwa na dhamana ya kuratibu mahusiano kati ya SECAM
na Taasisi mbali mbali zinazoongozwa na kusimamiwa na Umoja wa Afrika, ili kusaidia
mchakato wa maendeleo endelevu Barani Afrika mintarafu mwanga wa Waraka wa kichungaji
wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, Dhamana ya Afrika, "Africae Munus".
Bwana
Woldeyohannes kwa taaluma ni mwanasheria kutoka Chuo Kikuu cha Addis Ababa Ethiopia
ambako alijipatia shahada ya uzamili na baadaye akajiendeleza nchini Harare na huko
akajipatia shahada katika Falsafa. Ni mtaalam aliyebobea katika masuala ya ulinzi,
usalama na amani. Amewahi pia kufundisha maadili nchini Ethiopia pamoja na kuendeleza
shughuli za kichungaji za Kanisa Katoliki miongoni mwa vijana, nchini Ethiopia.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.