Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni baada ya kufanya mazungumzo na Kardinali Angelo
Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu,
ameridhia uamuzi uliofanywa na wajumbe wa Baraza hili la kipapa la kumtangaza Mtakatifu
Gregori wa Narek, kuwa Mwalimu wa Kanisa.
Mtakatifu huyu alikuwa ni Mtawa,
aliyezaliwa huko Andzevatsik, wakati huo ukijulikana kama Armenia ambayo ndiyo nchi
ya Uturuki kwa sasa. Ni mtawa na mwanataalimungu mahiri, aliyejipambanua kwa maandishi
na mtunga mashahiri maafuru; alikuwa mwaminifu na mtiifu kwa Mapokeo ya Mama Kanisa,
akaonesha bidii na heshima kubwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu. Inasadikiwa kwamba,
Bikira Maria alimtokea Mtakatifu Gregori.
Kati ya kazi zake kuu ambazo wengi
wanazikumbuka ni kuhusu "Hotuba ya Masifu kwa Bikira Maria" pamoja na Sala 80 ambazo
zilipewa jina, "Kutoka katika undani wa moyo wangu, majadiliano na Mama wa Mungu".
Sehemu hii ya sala inaonesha jinsi ambavyo Mtakatifu Gregori baada ya kukabiliwa na
magumu pamoja na machungu ya maisha yaliyomkatisha tamaa, mwishoni alifanikiwa kuona
upendo kutoka kwa Bikira Maria, akatambua msaada wake wa daima. Gregori wa Narek alifariki
dunia kunako mwaka 1005.
Kanisa nchini Armenia kwa miaka mingi lilikuwa linamtambua
kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Alitambulika na Mama Kanisa kutokana na utakatifu uliojikita
katika mafundisho makuu ya imani kama anavyokumbukwa katika Orodha ya Watakatifu wa
Kanisa, tarehe 27 Februari. Baba Mtakatifu Francisko wakati wowote kuanzia sasa anaweza
kumtangaza rasmi kuwa ni Mwalimu wa Kanisa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.