2015-02-24 12:22:35

Ile fedha, iwasaidie maskini!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Sri Lanka, Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Colombo, lilimpatia zaidi ya Millioni 8. 7 fedha ya Sri Lanka ili kuchangia mfuko wa mshikamano wa upendo unaotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amemrudishia fedha hii ambayo ni sawa na Euro zaidi ya 57, 000 Kardinali Malcolm Ranjith, ili zichangie huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii nchini Sri Lanka.

Ukarimu huu ulimgusa sana Baba Mtakatifu Francisko kiasi cha kusema kwamba, hata maskini katika umaskini wao ni wadau wakuu wa Uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Baba Mtakatifu anamwomba Kardinali Ranjith kumpatia maelezo ya kina jinsi fedha kwa ajili ya kuwasaidia maskini ilivyotumika.

Taarifa zinaonesha kwamba, fedha hii imegawanywa kwenye Majimbo mbali mbali nchini Sri Lanka ili kuwasaidia maskini kama changamoto ya ujenzi wa mshikamano wa utandawazi unaojali na kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.